Habari za Kitaifa

Shirika kufadhili vijana kibiashara hadi shilingi milioni moja

Na WINNIE ONYANDO August 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

VIJANA walio na mpango wa kuanzisha biashara katika sekta za kilimo, ufugaji na utalii sasa wanaweza kupata ufadhili kutoka kwa mashirika

Ili wanufaike na mpango wa serikali na mashirika mengine, vijana hawa wanahitaji kuwa katika vikundi vilivyosajiliwa.

Ufadhili huo unatolewa na Wakfu wa Stop Child Soldiers Foundation lililoanzishwa na Peter Juma Abass kutoka Sudan.

Kulingana na Bw Abass, ufadhili huo unalenga kuwanufaisha sio tu vijana wanaotoka katika nchi zinazokabiliwa na ukosefu wa usalama na amani bali pia vijana kutoka Kenya.

“Tunalenga kuwainua vijana kimapato ili waweze kujitegemea,” akasema Bw Abass.

Ili kupata ufadhili, sharti uwe kwenye kikundi au chama kilichosajiliwa na serikali na kikundi hicho pia sharti kiwe na ajenda inayoeleweka.

“Baada ya kupokea ombi lao, tuna timu ambayo tutatuma ili kukagua ikiwa vijana hao wanahitaji usaidizi kweli na pia kudhibitisha ikiwa kundi hilo ni la kuaminika,” akaongeza.

Kando na hayo, ikiwa kundi hili linataka kujihusisha katika suala la ufugaji, basi sharti liwe na shamba.

“Kazi yetu sasa itakuwa ni kukagua ombi lao kisha ikiwa wamehitimu matakwa yetu watapewa ufadhili.”

Shirika hilo linatoa ufadhili wa kati ya Sh50,000 na Sh1 milioni kwa kutegemea mahitaji ya wahusika.