Shule kuanza rasmi likizo fupi Jumatano huku ikigongana na maandamano
WAZIRI wa Elimu Ezekiel Machogu, jana alitangaza kuwa likizo fupi itaanza kesho hadi Jumatatu ijayo.
Akizungumza na Taifa Leo, Bw Machogu, alisema kuwa shule zitaanza kuwaruhusu wanafunzi kurejea nyumbani kuanzia kesho.
“Sijatangaza kuwa likizo fupi inaanza mnamo Jumatatu (jana) jinsi ambavyo inaripotiwa mitandaoni. Kwa mujibu wa kalenda ya masomo, likizo fupi inaanza Jumatano hadi Jumatatu ijayo,”akasema Bw Machogu.
Ingawa hivyo, alisema kuwa likizo hiyo ni kwa hiari na wanafunzi wanaweza kusalia shuleni bila kuenda nyumbani.
“Likizo fupi si lazima na inategemea mapenzi ya mzazi, shule na wanafunzi wenyewe ambao wanaweza kuamua kubakia shule ili kudurusu. Hata hivyo, tarehe rasmi inaanza Jumatano.”
Baadhi ya wazazi walieleza kero yao mitandaoni kuhusu hatua ya baadhi ya shule kutangaza kuwa likizo hiyo ingeanza Jumapili usiku.
Wazazi walisema walipokea jumbe kwenye simu zao zilizowataka wawachukue watoto wao na kwenda nao nyumbani kwa likizo hiyo.
Likizo hiyo ilikuwa ianze Juni 24, 2024 hadi Juni 26 ili kuwaruhusu walimu wakuu wa shule za upili kuhudhuria kongamano lao la kila mwaka jijini Mombasa.
Wiki chache zilizopita, tarehe hiyo ilibadilishwa kutokana na mkutano ambao uliandaliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili (KESSHA), Bw Willy Kuria, Bw Machogu na washikadau katika sekta ya elimu.
Mabadiliko hayo yaliisukuma tarehe hiyo hadi Juni 26 kutokana na mkutano huo wa walimu wakuu Mombasa. Naibu Rais Rigathi Gachagua anatarajiwa kufungua rasmi kongamano hilo hapo kesho.
Kalenda ya masomo ya mwaka huu ilivurugika kutokana na mafuriko makubwa ambayo yalishuhudiwa nchini. Janga hilo lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 200 na kuwaacha maelfu wengine bila makao.
Mafuriko hayo ndiyo yalichangia kusukumwa mbele kwa tarehe za kufungua shule kwa muhula wa pili na ule wa tatu. Hata hivyo, ratiba ya mtihani wa shule za upili ambao unaanza mnamo Novemba haikuvurugwa.
Mwanzoni shule zote zilistahili kufunguliwa Aprili 29, 2024 kwa muhula wa pili. Hata hivyo, ufunguzi huo ulisukumwa mbele hadi Mei 6 kutokana na mafuriko.
Baadaye Rais William Ruto alitangaza kuwa ufunguzi wa shule ulikuwa umeahirishwa kwa muda usiojulikana. Kalenda ya mwaka huu ya masomo inasema muhula wa kwanza ulikuwa wa wiki 13 kutoka Januari 8 hadi Aprili 5.
Muhula wa pili ambao ndio mrefu zaidi ulistahili kuanza Aprili 29 kwa wiki 14 hadi Agosti 2. Baadaye wanafunzi wangeenda likizo ya siku tatu kuanzia Juni 20 hadi Juni 23.
Hata hivyo, mpango huo ulibadilika na likizo fupu ikasongeshwa mbele kutoka Juni 26 hadi Julai 1, 2024 kutokana na kongamano la kila mwaka la walimu.