Sichezi mtakiona, Ruto aonya upinzani akisitiza amri ya waporaji kupigwa risasi
Huku mashirika mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu, yakishutumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi katika maandamano ya hivi karibuni dhidi ya serikali, Rais William Ruto Jumamosi alisisitiza msimamo wake wa kuamuru watu kupigwa risasi mguuni, akiahidi kulinda maisha na mali za Wakenya kwa nguvu zote huku akilaumu upinzani kwa kuchochea vijana kuzua vurugu.
Rais Ruto alisema atachukua hatua kali dhidi ya wahalifu wanaolenga mali za watu, ikiwa ni pamoja na wizi na uporaji.
Aidha, alitaka viongozi wa kidini na wanasiasa wasitafsiri hatua kali dhidi ya waandalizi wa ghasia katika maandamano ambayo yamesababisha vifo kadhaa na uharibifu mkubwa wa mali, kama mateso ya kisiasa.
“Nimevumilia kwa muda mrefu sana, sasa imetosha. Wale mnaochochea vijana kuingia kwenye ghasia mtawajibika, msije mkasema ni mateso ya kisiasa,” alisema Rais Ruto wakati wa hafla ya kupanda miti huko Simotwo, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Alisema maandamano hayo yanalenga kudhoofisha serikali yake na akaonya upinzani na viongozi wa dini dhidi ya kuwalinda wahalifu wanaohusika na uharibifu wa mali wakati wa maandamano.
“Msitutishe kwa siasa. Tufanye kila juhudi kulinda maisha na mali ya Wakenya kwa gharama yoyote, kama ilivyoainishwa katika Katiba,” alisema Rais Ruto.
Rais alisema watu waliokamatwa kwa makosa ya kuharibu mali, ikiwa ni pamoja na kuchoma vituo vya polisi, mahakama, na mali binafsi katika Murang’a, Nyeri, Nakuru, Nairobi, Mombasa na maeneo mengine, watachukuliwa kama wahalifu na kushughulikiwa kisheria.
Alisisitiza kwamba kila mtu anayesababisha vurugu atakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria bila kujali hadhi yake ya kijamii.
“Sitakubali kurudi nyuma katika kuhakikisha maisha na mali za Wakenya inalindwa. Wakosoaji wangu wajitayarishe kupambana nami kwenye uchaguzi mkuu ujao,” aliongeza.
Rais Ruto alirudia kauli yake kuwa upinzani hauna ajenda kwa Wakenya na unawachochea vijana kuzua vurugu ili kufufua umaarufu wao wa kisiasa unaozidi kuporomoka.
Aliwahimiza Wakenya kuwahukumu viongozi kwa rekodi ya utendaji wao.
“Tuwahukumu viongozi kwa misingi ya utendaji wao. Nimeimarisha uchumi, nimeunda ajira kupitia mradi wa makazi, uchumi wa kidijitali, na soko la ajira za nje,” alisema Dkt Ruto.
Alisisitiza kuwa ana ajenda madhubuti ya kugombea tena urais mwaka wa 2027 na akautaka upinzani kujiandaa kwa mapambano makali ya kisiasa.
Pia, Rais Ruto alitetea Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), akisema kwamba tofauti na NHIF ya zamani, SHA itakuwa huru dhidi ya ufisadi na kuwawezesha Wakenya kupata huduma bora za afya.
“Nitahakikisha SHA haina ufisadi. Naomba Wakenya wajisajili ili kupata huduma bora za afya kupitia SHA,” alisema.