Habari za Kitaifa

Stella Lang’at akataliwa kuchukua wadhifa uliokuwa wa Aisha Jumwa

Na CHARLES WASONGA August 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KAMATI ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uteuzi imekataa kumwidhinisha Waziri Mteule wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi Stella Soi Lang’at kwa wadhifa huo.

Kwenye ripoti iliwasilishwa bungeni Jumatano alasiri, kamati hiyo iliyowapiga msasa mawaziri 20 wateule kwa siku nne wiki jana, hata hivyo, imeidhinisha uteuzi wa wengine 19.

Wabunge hao walifikia uamuzi wa kumkataa Bi Lang’at baada ya kutoridhishwa na uwezo na ufahamu wake wa masuala yanayohusu wizara aliyopendekezwa kuhudumu.

“Ijumaa wiki jana, alipofika mbele yetu, Bi Lang’at alionekana kama mtu asiyeelewa kabisa masuala yanayohusu Wizara hiyo licha ya kwamba yeye ni mwanamke. Mara sio moja alitatanika alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa wanachama wa kamati yetu. Hii ndio maana tumeamua kwa kauli kumkataa,” akasema Mbunge wa Saboti Caleb Amisi, ambaye ni mwanachama wa kamati hiyo.

Hata hivyo, kamati hiyo imeidhinishwa uteuzi wa mawaziri wateule wafuatao katika nyadhifa walizoteuliwa:

Profesa Kithure Kindiki (Usalama), Dkt Debra Barasa (Afya), Alice Wahome (Ardhi), Julius Migos (Elimu), Soipan Tuya (Ulinzi) na Eric Muuga (Maji).

Wengine ni pamoja na Aden Duale (Mazingira), Davis Chirchir (Barabara) Margaret Nyambura (ICT), John Mbadi (Fedha), Salim Mvurya (Biashara), Rebecca Miano (Utalii), Opiyo Wandayi (Kawi), Kipchumba Murkomen (Michezo), Hassan Ali Joho (Uchumi wa Baharini), Alfred Mutua (Leba), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika) na Justin Muturi (Utumishi wa Umma).

Endapo wabunge watakubaliana na mapendekezo ya kamati hiyo, Rais atahitajika kupendekeza mtu mwingine kwa Wizara ya Jinsia kuchukua mahala pa Bi Lang’at.

Aidha, atawateua rasmi mawaziri hao wateule 19 kutoa nafasi ya kuapishwa kwao na kuanza kuchapa kazi.