Habari za Kitaifa

Sudi avaa saa ya Sh17 milioni, asema iliundiwa binadamu si miti au ng’ombe

Na Elizabeth Ngigi na Winnie Onyando August 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Kapseret, Oscar Sudi amezua mjadala kwenye mitandao tofauti ya kijamii, baada ya kuonyesha saa yake ya mkono yenye thamani ya Sh17 milioni.

Saa hiyo ya kifahari ya Ulysse Nardin Freak Phantom, imezua mjadala mtandaoni, huku wakosoaji wakimshutumu mbunge huyo wakisema hana huruma akitembea na saa kama hiyo ilhali Wakenya wanalala njaa.

Bw Sudi alifichua kuwa saa hiyo ilikuwa zawadi kutoka kwa waziri mkuu wa zamani wa nchi nyingine.

“Nilikuwa na saa kama hizi mbili lakini hata sijui gharama yake kamili,” Bw Sudi alimwambia Oga Obinna wakati wa mahojiano.

Katika mahojiano hayo hayo, Bw Sudi alizungumzia maisha ya kifahari ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Bw Kipchumba Murkomen.

Alisema Bw Murkomen, ambaye amewahi kuwa mhadhiri, seneta, na sasa waziri, awali alitajwa kumiliki saa yenye thamani ya Sh900,000, ufichuzi uliozua mjadala kwenye mitandao ya kijamii.

“Murkomen amekuwa mhadhiri, seneta kwa mihula miwili, na waziri kwa miaka miwili, na alisema saa yake ina thamani ya Sh900,000. Kweli, Sh900,000 ni nini?” Bw Sudi alisema.

“Wakati mwingine Wakenya wanakosea. Saa kama hii haikutengenezewa miti au ng’ombe kuvaa; ilitengenezwa kwa ajili ya binadamu. Unataka nani avae saa kama hii? Tuache wivu,” akasema akitetea mtindo wake wa maisha.

Maoni ya Sudi yamezua hisia tofauti mtandaoni huku baadhi ya watu wakimtetea mbunge huyo wakisema kuwa utajiri wake na maisha yake ya kifahari yanatokana na bidii yake kwenye biashara.