Habari za Kitaifa

Tabasamu itarejea? Gachagua sasa arejeshewa walinzi wake

Na JUSTUS OCHIENG, STEVE OTIENO October 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI Jumapili ilimrejeshea Naibu Rais aliyeng’atuliwa Rigathi Gachagua walinzi wake na pia katika makazi yake rasmi ya Karen. 

Bw Gachagua alilalamika kuwa maisha yake yamo hatarini baada ya walinzi wake kuondolewa kufuatia kutimuliwa kwake na Bunge la Kitaifa na Seneti. Jana alihudhuria ibada katika Kaunti ya Kiambu akiwa na walinzi wake na kuandamana na wanasiasa wengi pamoja na mkewe Dorcas Rigathi.

“Serikali imemrejeshea naibu rais walinzi na sasa naomba rais iwarejeshe kazini walioajiriwa katika afisi yake ambao walitimuliwa. Lazima haki itendeke,” akasema Seneta wa Kiambu Karungo wa Thangwa.

Seneta huyo alikuwa kati ya viongozi ambao waliandamana na Bw Gachagua katika ibada hiyo katika Kanisa la Kianglikana la ACK Kiambu.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala ambaye alihudhuria ibada hiyo pia alithibitisha Bw Gachagua alirejeshewa walinzi wake.

“Ndiyo ni kweli,” akasema Bw Malala, seneta wa zamani wa Kakamega.

Jirani wa Bw Gachagua mtaani Karen pia alithibitisha kuwa alikuwa amerejeshewa walinzi.

“Nilikuwa naenda nyumbani ndipo nikasimamishwa na maafisa wa polisi ambao waliniuliza nilikokuwa nikienda. Baaada ya kujitambulisha waliniruhusu na mmoja wa afisa hao aliniambia walikuwa walinzi katika boma la naibu rais,” akasema jirani.

Alifichua kuwa baadaye walinzi hao waliondoka tena. Kwenye ibada ya jana, Bw Gachagua aliandama na wandani wake hasa kutoka Mlima Kenya ambao walisisitiza kuwa bado wapo nyuma yake na masaibu ya kisiasa anayoyapitia yataisha.