Tanzania yafurusha maelfu ya wafugaji kutoka Kenya
SHIRIKA moja la kimataifa la kutetea haki za kibinadamu linalalamikia hatua ya serikali ya Tanzania kuwafurusha maelfu ya wafugaji kutoka Kenya waliokuwa wakiendeleza ufugaji nchini humo.
Wafugaji hao wamekuwa wakiishi katika ardhi yao ya kijamii.
Katika ripoti ya Human Rights Watch iliyotolewa mnamo Jumatano, Julai 31, 2024, shirika hilo lilidai kwamba walinzi wa pori waliwatandika baadhi ya wafugaji wa jamii hiyo bila kuzingatia sheria.
Ripoti ya shirika hilo ilieleza jinsi waathiriwa walilengwa, na pia kuorodhesha visa 13 vya kupigwa kati ya Septemba 2022 na Julai 2023.
Human Rights Watch ilisema mvutano wa muda mrefu kati ya mamlaka na jamii ya wafugaji hao wakati mwingine husababisha vita baada ya serikali mnamo 2022, kuanzisha mpango wa kuhamisha karibu watu 82, 000 kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kuwapeleka wilayani Handeni, takriban kilomita 600.
Shirika hilo la kutetea haki za kibinadamu pia limesema liliwahoji watu 100 kati ya Agosti 2022 na Desemba 2023, pamoja na wanajamii ambao tayari walikuwa wamehamishiwa katika kijiji cha Msomera, Handeni na wengine wanaosubiri kuhamishwa.