Habari za Kitaifa

Tutaokoa Chuo Kikuu cha Moi kisisambaratike, Waziri Ogamba aahidi

Na WYCLIFFE NYABERI November 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Elimu Julius Ogamba amesema serikali itakiokoa Chuo Kikuu cha Moi kisianguke.

Waziri huyo amedokeza kuwa juhudi za kufufua taasisi hiyo ziko katika hatua za mwisho na hivi karibuni, watatangazia umma kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kurejesha shughuli za masomo katika taasisi hiyo.

Akizungumza alipokuwa akikagua jinsi mtihani wa KCSE ulivyokuwa ukiendelea Jumatatu, Novemba 18, 2024 baada ya kuzuru kaunti za Kisii na Nyamira, Bw Ogamba alisikitishwa na hali inayokikumba chuo hicho lakini akaeleza matumaini yake kuwa hivi karibuni taasisi hiyo itainuka.

“Tumeweka mpango wa kuhakikisha kuwa tunaendeleza chuo hicho. Tumebuni mkakati wa kushughulikia masuala yanayokiathiri na tutawajuza mara tu mikakati hiyo itakapokamilika,” Bw Ogamba alisema.

Mambo hayajawa sawa kwa taasisi hiyo yenye makao yake mjini Eldoret kwani imekuwa ikigonga vichwa vya habari katika siku za hivi karibuni kwa taarifa za kuvunja moyo.

Chuo hicho kimelemewa na madeni, maamuzi mabaya ya kifedha na kiutawala, nguvu kazi isiyoweza kumudiwa, miradi potovu na mengine mengi.

Waziri Julius Ogamba (kushoto) afurahia picha na walimu wakati wa kukagua mtihani wa KCSE kaunti za Kisii na Nyamira. Picha|Wycliffe Nyaberi

Ina madeni ya zaidi ya Sh8 bilioni na wahadhiri wako kwenye mgomo, wakipinga mishahara kucheleweshwa, kutotumwa kwa malipo ya mikopo, pensheni na makato mengine ya watu wengine.

Wahadhiri hao wanataka kulipwa zaidi ya Sh8 bilioni, ikiwa ni pamoja na malimbikizo ya mishahara na fedha nyingine wanazodai kabla ya kurejea kazini.

Juhudi za kumaliza mgomo huo zimefeli huku wahadhiri hao wakishutumu uongozi wa chuo kwa kutowajali.

Kufuatia vuta nikuvute hiyo, wanafunzi ndio walioumia zaidi. Kwa sababu ya migomo isiyoisha ya wahadhiri hao, wanafunzi wanachukua miaka mingi kumaliza masomo yao katika muda unaostahili.

Waziri Ogamba katika bohari la mtihani. Picha|Wycliffe Nyaberi

“Sio haki kwa wanafunzi kwenda chuo kikuu kwa mfano na kukaa kwa miaka tisa katika mchakato wa kufanya digrii zao. Si sawa na tunaenda kupata suluhu za muda mrefu na za kudumu kwa chuo hicho,” Bw Ogamba aliongeza.

Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa, inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly ilizuru taasisi hiyo hivi majuzi na kutaka usimamizi ya chuo hicho uvunjiliwe mbali.

Kamati ilipendekeza uongozi wa taasisi hiyo uwekwe chini ya ushikilizi. Bw Ogamba alisema Wizara yake itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa sekta ya elimu inaboreshwa.

Alisema hilo litaanza kwa kuhakikisha wanakomesha utamaduni wa kufanya udanganyifu katika mitihani. Aliwataka maafisa wanaosimamia mtihani unaoendelea kutolegeza kamba kwani mtihani huo unakaribia kufika tamati baadaye wiki hii.