Tutaungana kukomboa Kenya kutoka utawala wa Ruto, asema Gachagua
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amehimiza ushirikiano wa viongozi wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 kuikomboa nchi kutoka kwa ‘utawala mbaya’ wa Rais William Ruto.
Akizungumza baada ya ibada ya Jumapili katika kanisa la Gospel Confirmation Centre Mjini Machakos, Bw Gachagua alieleza imani kwamba kutakuwa na muungano thabiti kati yake na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.
“Jambo muhimu zaidi ni kwa eneo la Mlima Kenya kuungana na ngome za Bw Musyoka. Tukiungana kama eneo, tunaweza kwenda maeneo mengine kama kapu moja la kura. Tutatembea pamoja safari hii,” alisema.
Aliongeza: “Muungano kati ya wapiga kura wa Mlima Kenya na wapiga kura wa kaunti za kusini mashariki unaweza kutawala nchi hii kwa miaka 100 ijayo”.
Naibu Gavana wa Machakos, Francis Mwangangi, alisema viongozi wa upinzani wakigawanyika Rais Ruto atachaguliwa tena.
“Bw Gachagua una ufunguo wa kuikomboa nchi hii. Hakikisha unaungana na Bw Musyoka. Tuliona enzi za Rais Daniel Moi na upinzani usio na umoja unaweza kuhakikisha kuwa Rais Ruto anachaguliwa tena,” akasema huku akimsihi Bw Gachagua kuhakikisha kuwa ushirikiano wakena Bw Musyoka unadumu.
Maseneta John Kinyua (Laikipia), Karungo Thangwa (Kiambu), Daniel Maanzo (Makueni), Enoch Wambua (Kitui), Agnes Kavindu (Machakos), na Joe Nyutu (Murang’a) walisema waliidhinisha umoja wa Bw Musyoka na Gachagua.
“Kama eneo la Mlima Kenya tuko nyuma kabisa ya Bw Gachagua. Tumemruhusu kuungana na Bw Musyoka kukomboa nchi hii. Hatujali iwapo Raila Odinga atajiunga nao au la. Wana kile kinachohitajika kukomboa nchi hii kutoka kwa utawala mbaya wa Rais Ruto,” alisema Bw Kinyua.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wabunge washirika wa Bw Gachagua na Bw Musyoka, Bw Wambua alisema: “msikubali kugawanyika kwa sababu ya kung’ang’ania mamlaka.”