Habari za Kitaifa

Uamuzi katika kesi ya kung’oa Rigathi unaomtishia Koome

Na JOSEPH WANGUI February 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MZOZO unaoendelea kuhusu kuondolewa afisini kwa majaji saba wa Mahakama ya Juu, akiwemo Jaji Mkuu Martha Koome, umechukua mkondo mpya baada ya mmoja wa walalamishi kuitaka mahakama hiyo kutupilia mbali maagizo ya muda yaliyositisha mchakato huo akitaja uamuzi uliotolewa wakati wa kutimuliwa kwa naibu rais Rigathi Gachagua.

Wakili Nelson Havi anasema mchakato wa Kikatiba hauwezi kusitishwa na maagizo hayo ya muda.Anasema ni sawa na kusitisha kipengele cha katiba na kuzuia Tume ya Utumishi wa Mahakama kufanya kazi zake.

Anataka mahakama kutupilia mbali maagizo hayo ya muda.Amekita ombi lake katika uamuzi wa kesi ya kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua dhidi ya Bunge la Kitaifa ambapo Mahakama ya Juu iliamua kwamba mchakato wa katiba unapoendelea hauwezi kusitishwa au kuingiliwa.

Katika kesi hiyo, mahakama ilisema kwamba “kutoa amri ya kusimamisha kifungu cha katiba kungekiuka kanuni moja kwa moja, kwa kuweka uamuzi wa mahakama juu ya sheria kuu za nchi”.

“Ikiwa Mahakama ya Juu haikuwa na uwezo wa kuzuia Bunge kushughulikia hoja ya kuondolewa kwa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya, bila shaka haiwezi kuwa na uwezo wa kuzuia JSC kushughulikia ombi la kuondolewa kwa Majaji saba wa Mahakama ya Juu,” akasema Bw Havi.

Amewasilisha ombi mahakamani akikosoa kesi ya Bw Pariken Ole Esho, kupinga uamuzi wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) wa kuwataka majaji kujibu shutuma zinazowakabili.

Pia anataka kesi hiyo ihamishwe kutoka Mahakama Kuu ya Narok hadi Kitengo cha Masuala ya Katiba katika Mahakama Kuu jijini Nairobi na kufutiliwa mbali kwa kesi iliyowasilishwa na Bw Pariken Ole Esho.

Anataka kesi yake iidhinishwe na kusikilizwa haraka.“Bw Ole Esho aliomba na akapewa maagizo ya kuzima JSC kutekeleza kazi yake ya kikatiba ya kuzingatia maombi ya kuondolewa kwa majaji saba wa Mahakama ya Juu,” asema Bw Havi, ambaye pia ni rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Kenya.

Amesikitishwa na maagizo ya muda yaliyotolewa na Jaji Charles Kariuki mnamo Jumatano kuzuia JSC kuendelea na malalamishi matatu ya kuwaondoa afisini majaji wa mahakama ya juu kwa madai ya utepetevu na utovu wa nidhamu. Maagizo hayo yataendelea kutumika hadi kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na Bw Ole Esho.

“Majaji saba wa Mahakama ya Juu hawajapinga agizo la kujibu kesi ya kuondolewa kwao,” alisema Bw Havi.Katika kushinikiza kesi kuhamishwa hadi Nairobi, Bw Havi alisema kuwa mahali pafaapo pa kuwasilisha malalalamishi ni Mahakama Kuu ya Kenya iliyoko Nairobi, Kitengo cha Masuala ya Katiba.

Malalamishi dhidi ya majaji wa mahakama ya juu katika JSC yaliwasilishwa na Bw Havi, kampuni ya Dari Limited ya aliyekuwa waziri Raphael Tuju na wakili Christopher Rosana.