Uamuzi wa korti uliopatia Azimio la Umoja ushindi muhimu
MUUNGANO wa Azimio la Umoja One Kenya, jana ulipata ushindi muhimu kortini baada ya majaji kuamua kuwa, una idadi kubwa ya wabunge na unapaswa kuwa wa walio wengi.
Mahakama Kuu iliharamisha uamuzi wa Spika Moses Wetang’ula ambapo alitangaza muungano wa Rais William Ruto wa Kenya Kwanza kuwa wa walio wengi katika Bunge la kitaifa.
Majaji Jairus Ngaa, John Chigiti na Lawrence Mugambi walisema matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 2022 yalionyesha kwamba, mrengo wa Azimio ndio uliokuwa na wabunge wengi.
Majaji hao walisema Bw Wetang’ula alikiuka Katiba kwa kutoa uamuzi huo kinyume cha sheria na bila ya kuwa na ushahidi.
Wakitoa uamuzi katika kesi iliyowasilishwa na makundi 12 ya kutetea haki za binadamu chini ya mwavuli wa vugu vugu la “wananchi na wapiga kura wa Kenya” majaji hao walisema kwamba, hakuna ushahidi kuunga mkono madai kwamba vyama vitano vya kisiasa vilikuwa vimeuhama mrengo wa Azimio ulioongozwa na Raila Odinga kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza.
Majaji hao walisema hakuna mikataba iliyotiwa sahihi na kupelekewa Msajili wa Vyama kuthibitisha vyama hivyo vilikuwa vimehama kirasmi kutoka muungano wa Azimio kujiunga na Kenya Kwanza baada ya uchaguzi mkuu.
Majaji hao walivitambua vyama hivyo kuwa-Movement for Democracy and Growth (MDG) chake Mbunge wa Ugenya Bw David Ochieng, United Democratic Movement (UDM) cha Seneta wa Mandera Ali Roba, Pamoja African Alliance (PAA) chake Spika Amason Kingi’ , Chama Cha Mashinani (CCM) cha aliyekuwa Gavana wa Bomet Bw Isaac Ruto na chama cha Maendeleo Chap Chap, cha Dkt Alred Mutua.
“Kwa kutambua wabunge 14 kutoka vyama vya MDG, UDM, PAA, CCM na MCCP na kutangaza walikuwa wamejiunga mrengo wa Kenya Kwanza (KK) bila ushahidi wa mikataba ya baada uchaguzi mkuu wa Agosti 9,2022 na kuutangaza mrengo wa Kenya Kwanza kuwa walio wengi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alikaidi Kifungu nambari 101 cha Katiba,”majaji hao waliamua.
Majaji hao walifutilia mbali na kuharamisha uamuzi huo wa Spika Bw Wetang’ula wa Oktoba 6, 2022 wakisema hauna mashiko kisheria na kikatiba. “Baada ya kushtakiwa, Bw Wetang’ula aliwasilisha hati ya kiapo mahakamani na hakuthibitisha kwamba kulikuwa na mikataba iliyotiwa sahihi kati ya vyama hivyo vitano na Kenya Kwanza.
Hakuna ushahidi kwamba, vyama hivi viliuhama muungano wa Azimio kujiunga na Kenya Kwanza. Vyama hivi havikutimiza mahitaji ya Sheria nambari 109 ya Vyama vya Kisiasa,” mahakama ilisema.
Majaji hao walisema uamuzi wa Spika Wetang’ula ulipotoka na kukaidi Katiba na sheria.Mzozo huo ulitokana na barua mbili alizopokea Wetang’ula Oktoba 4,2022 kutoka kwa Azimio na Kenya Kwanza ziking’ang’ania uongozi wa walio wengi.
Ushahidi uliowasilishwa kortini ulithibitisha Azimio ina wabunge 171 na Kenya Kwanza 165. Kupitia wakili Kibe Mungai, walalamishi waliomba mahakama iharamishe uamuzi wa Spika Wetang’ula kutambua Kenya Kwanza mrengo wa wengi na Azimio mrengo wa wachache.
Jana, vinara wa Azimio Kalonzo Musyoka na Eugene Wamalwa walisema uamuzi huo ni ithibati tosha kwamba Rais William Ruto ameiteka Bunge.“Sasa Ruto ameanikwa na huu ndio ukweli. Kwa hivyo, si aheshimu uamuzi wa mahakama na aruhusu muungano wa walio wengi uchukue nafasi yake katika Bunge?” akasema Bw Musyoka.
Bw Wamalwa alitaja uamuzi huo kama wenye umuhimu mkubwa kuwahi kutolewa na Mahakama katika siku za hivi karibuni.
“Ni uamuzi mkuu unaobatilisha maamuzi mabaya kuwahi kutolewa na bunge letu-chini ya usimamizi wa Spika mwenye mapendeleo zaidi katika historia ya taifa hili, Moses Wetang’ula,” akasema waziri huyo wa zamani wa Ulinzi.
Kulingana na Bw Wamalwa, spika ni kama refa ambaye anatarajiwa kutopendelea upande wowote, ilhali Wetang’ula amekuwa akipendelea upande mmoja.