Uhuru aunga mkono azma ya Raila ya AUC
AFISI ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta imesema anaunga mkono azma ya Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) huku ikiibuka kuwa Bw Kenyatta anawafikia marafiki wake wa zamani kumsaidie kiongozi huyo wa Azimio.
Msemaji wa rais huyo mstaafu Kanze Dena Mararo alisema licha ya kutohudhuria hafla ya kuzindua rasmi kampeni za Odinga wiki jana, anamtakia ushindi.
“Mheshimiwa Rais yuko nje ya nchi na ndio maana hakuhudhuria uzinduzi huo. Lakini anaunga mkono kikamilifu azma ya Rais,” akasema Bi Kanze.
Sherehe hiyo ya uzinduzi wa Bw Odinga iliongozwa na Rais William Ruto, huku mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit akiwaongoza marais wa ukanda huo kumwidhinisha Bw Odinga kwa wadhifa huo.
Marais Yoweri Museveni (Uganda) na Samia Suluhu Hassan (Tanzania), walihudhuria hafla hiyo katika Ikulu ya Nairobi.
Wengine walikuwa Waziri Mkuu wa Burundi Gervais Ndirakobuca na mwakilishi wa Rais wa Rwanda Paul Kagame – Waziri wa Masuala ya Kigenmi James Kabarebe.
Pia, walikuwepo marais wa zamani Jakaya Kikwete wa Tanzania na mwenzake wa Nigeria, Olusegun Obasanjo.
Bw Kenyatta aliyemuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi wa urais 2022, hakuhudhuria, na hivyo kuibua maswali mengi.
Vile vile, vinara wa Azimio wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka walichelea kuhudhuria hafla hiyo ya kufana.
Katika shughuli hiyo, Rais Ruto alimtaka Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Koriri Sing’oei na aliyekuwa Balozi wa Kenya Amerika, Elkana Odembo kuongoza sekritariati ya kushirikisha kampeni za Bw Odinga.
Bw Odembo aliambia Taifa Dijitali kwamba Bw Kenyatta amekuwa akiunga mkono kampeni za Odinga na amewafikia baadhi ya marafiki zake kumpigia debe mgombeaji huyo wa Kenya.
“Rais wa zamani anaelewana zaidi na baadhi ya marais wa Afrika na ni mmoja wa wale tunaoshirikiana nao kuwafikia marais watakaoshiriki uchaguzi wa mwenyekiti wa AUC Februari 2025,” Bw Odemba akasema.
Bw Odinga atakabiliana na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Youssouf, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Mauritius, Anil Kumarsingh Gayan na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni Madagascar, Richard James Randriamandrato.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga