Ukatili SHA ikiendelea kutesa wagonjwa wa saratani wakiambiwa warudi mwaka ujao
MAMIA ya wagonjwa wa saratani nchini wanahangaika kupata matibabu kwa ufadhili wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), hatua ambayo wengi wanataja kuwa ya kikatili.
Gatamu Waigwa, mkazi wa Nyeri mwenye umri wa miaka 70, ni miongoni mwa waathiriwa wa mabadiliko hayo. Kwa miezi minne sasa, amekuwa akisafiri kila siku kutoka Nyeri hadi Nairobi kuomba msaada wa kupata dawa muhimu za saratani.
Awali, NHIF ilifadhili matibabu yake kwa Sh600,000 kwa mwaka, lakini SHA imepunguza kiwango hicho hadi Sh400,000 na kumsukuma katika hatari ya kupoteza maisha kwa kukosa dawa.
SHA pia imeshindwa kuheshimu ahadi ya kufadhili matibabu ya saratani kwa Sh550,000. Aliambiwa asubiri hadi mwaka ujao wa kifedha ili apate huduma tena jambo linalopingwa vikali na wahudumu wa afya na watetezi wa haki za wagonjwa.
Kwa sasa, wagonjwa wengi wa saratani wanalazimika kufanya harambee, kuuza mali, au kuacha matibabu kutokana na ukosefu wa fedha. Mfumo wa SHA unalaumiwa kwa ukosefu wa uwazi na ufanisi.
Wito umetolewa kwa Rais William Ruto na Waziri wa Afya Aden Duale kuchukua hatua za dharura kurejesha matumaini kwa wagonjwa waliokwama kutokana na mfumo mpya wa SHA.