Habari za Kitaifa

Ukusanyaji maoni ya umma kuhusu Gachagua wazua maswali ya kisheria

Na SAMWEL OWINO October 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MIKUTANO ya ushirikishaji wa umma kuhusu hoja ya kumbandua Naibu Rais Rigathi Gachagua inayoanza leo imeibua mategu mengi ya kisheria.

Shughuli hiyo inatarajiwa itafanyika katika maeneobunge yote 290 na kisheria inastahili kuendeshwa na wafanyakazi wabunge. Hoja ya kumtimua Naibu Rais inatarajiwa kujadiliwa bungeni mnamo Jumanne ijayo.

Licha ya shughuli hiyo kuendelezwa leo kwa sababu ni lazima kisheria, maswali yameibuka iwapo matokeo yake yatazingatiwa au kuheshimiwa. Baadhi ya wabunge jana walisema shughuli hiyo inaendelezwa kutimiza tu hitaji la kisheria japo hatima ya Bw Gachagua ishaamuliwa.

Hapo awali, Bunge la Kitaifa limejipata pabaya baada ya baadhi ya miswada yake kuangushwa kutokana na kukosekana kutekelezwa kwa mikutano ya ushirikishaji wa umma.

Mbunge wa Gatanga Wakili Edward Muriu Alhamisi alisema ushirikishaji wa umma utafanya wabunge wawe na ufahamu kuhusu kile ambacho raia wanakitaka wakati wa kujadiliwa kwa mswada huyo.

Pia alisema matokeo au maoni ya raia ndiyo yataamua iwapo Bw Gachagua anangátuliwa au anasalia madarakani.

“Inatarajiwa wabunge wakijadili hoja hiyo basi watakuwa wamefahamu kile ambacho raia wanataka kutokana na ripoti ya mwisho,” akasema Bw Muriu.

Hata hivyo, maswali yameibuka kuhusu idadi ya watu ambao wanahitajika kushiriki huku suala hilo likiwapa wanasiasa nafasi ya kuwasafirisha wafuasi wao mahali ambapo fomu hizo zitakuwa zikitiwa saini.

Bunge lilisema kuwa hakuna idadi kamili ya raia ambao wanastahili kujaza fomu hiyo.

“Mahakama imeagiza kuwa mikutano ya ushirikishaji wa umma lazima izingatie vigezo na viwango vinavyohitajika kisheria,” ikasema Bunge.

Huku utata ukizidi kuhusu idadi ya watu ambao watajitokeza kwenye maeneobunge, wafanyakazi wabunge pia imebainika hawana data ya kuthibitisha maelezo ya aliyejaza fomu hiyo.

Hii ni kinyume na wakati wa kura ambapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) ina sajili ya wapigakura na hufanya ukaguzi kabla ya mtu kuruhusiwa kuchaguana.

Kwa hilo la Bw Gachagua mtu anaweza kuchukua fomu nyingi jinsi anavyotaka kisha awape wafuasi wake na waandike kuwa wanapinga hoja hiyo.

“Iwapo watu watakataa hoja hiyo basi kama mbunge huwezi kuenda kinyume na uamuzi wa waliomchagua. Ukienda kinyume na hilo basi watakugeuka na kusema wewe si mwakilishi wao,” akasema Bw Muriu.

Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru maarufu kama Mejjadonk naye alishanga iwapo bunge lina rasilimali za kuendesha ushirikishaji wa umma.

Bw Gathiru na mwenzake wa Kitui cha Kati Makalo Mulu pia walishangaa kwa nini baadhi ya wabunge walipokezwa hela za kugharimia ushirikishaji wa umma katika maeneo yao huku wengine wakiachwa nje.

“Pesa hizo zilikuwa na malengo ya kuwashawishi kisiasa. Tulimkabili karani kwa nini hela hizo zilitolewa tu kwa watu ambao walitia saini hoja ya kumtimua Naibu Rais,” akasema Dkt Mulu.