Uraibu wa michezo ya kamari unavyozamisha vijana
KATIKA mitaa ya mabanda jijini Nairobi, uraibu wa kamari ni janga linalopanuka likichochewa na simu na maduka ya kutoa huduma hizo.
Vijana wengi wamevutwa na ndoto ya kupata pesa kwa haraka, wakitumai kuwa kamari itawatoa katika umasikini.
Kwa baadhi yao, ni ndoto; kwa wengine, ni jinamizi ambalo tayari limeharibu maisha yao.
Ajira, mahusiano na hata uhusiano wa kifamilia zinaporomoka.
Kile kilichoanza kama matumaini kimegeuka kuwa mzunguko wa kukata tamaa.
Katika mitaa ya Kangemi na Kawangware yenye watu wengi jijini, kuna zaidi ya maduka 60 ya kamari.
Pembeni mwa maduka haya, wakopeshaji wa riba wameweka vibanda vyao ili kutoa mikopo ya haraka kwa watu wanaotaka kuwekeza katika kamari.
Wengi wa wateja ni vijana wanaume walio wa umri wa kati ya miaka 20 na 30, lakini wahudumu wa maduka haya mara nyingi ni wanawake.
Kwa vijana hawa, kamari inaonekana kama tiketi yao ya maisha bora. Ndoto ni rahisi: kushinda beti kubwa, kupiga teke maisha magumu, na kuishi kwa uhuru wa kifedha.
Lakini kwa wengine, si suala la bahati tena—ni kutekwa na uraibu wa kamari, jambo ambalo linafyonza pesa na kuacha uharibifu mkubwa.
“Nilikuwa na familia, lakini ilipotea kwa sababu ya kamari,” anasema Wycliffe Olunyi, aliyekuwa mcheza Kamari.
Olunyi ana umri wa miaka 30.
“Nilikuwa na kazi nzuri huko Upper Hill, lakini kamari ilimeza kila kitu.”
Katika jiji la Nairobi, wengi wamepitia hali kama yake. Kwa wengine, kama Isabel Akinyi, mwenye umri wa miaka 23, aliyekuwa mteja wa kamari na sasa anajitahidi kulea mtoto wake, kamari ilimletea uharibifu.
“Nilikuwa nacheza kamari, lakini baada ya kupata mtoto, nililazimika kuacha. Baba wa mtoto wangu pia amenaswa kwenye kamari,” anasema, huku macho yake yakionyesha uchungu wa matumaini yaliyopotea.
Athari za uraibu wa kamari ni zaidi ya kifedha; zinakumba hisia na hali ya kiakili ya wahusika. Daniel mwalimu mwenye umri wa miaka 30 anajua hili vyema.
Maisha yake ni ushuhuda wa jinsi uraibu wa kamari unavyoweza kuangamiza hata mtu aliyekuwa na mustakabali mzuri.
Daniel anaeleza jinsi maisha yake yalivyobadilika alipostaafu na kupokea malipo yake—Sh 200, 000 alizochukulia kama mwanzo wa maisha bora.
“Nilikuwa mimi, simu yangu, na kitanda changu. Ndani ya wiki mbili, nilibaki na Sh3, 000 tu,” anakumbuka, macho yake yakionyesha majuto.
Licha ya jitihada zake za kuacha kamari, Daniel alijikuta akirudi tena kwenye mtego huo.
“Nafanya kazi yangu vizuri, lakini pesa zinapoingia, nabadilika kabisa. Huwezi kunidhibiti,” anakiri.
Kwa Daniel, kamari ilikuwa njia ya kukabiliana na matatizo ya maisha na hamu ya kuepuka maisha ya kawaida yasiyo na msisimko.
“Ni hisia kali sana. Unapohisi umesononeka, unadhani kamari ndiyo njia pekee ya kukuokoa,” anaeleza.
Mwanasaikolojia, Ken Peter Munywa anasema kuwa watu wengi huingia kwenye kamari wakiamini kuwa ni njia ya kutatua matatizo yao ya kifedha na msongo wa mawazo.
“Baadhi huona kamari kama suluhisho la shida zao—shida za nyumbani, au matatizo ya kifedha. Wanatumaini kuwa kupitia kamari, maisha yao yatabadilika. Lakini kama uraibu wowote, mambo huweza kuharibika haraka sana,” anasema.
Kwa watu kama Daniel, safari ya kupona ni ndefu na imejaa vishawishi.
“Nimejaribu kuacha, lakini bado nahitaji msaada. Wenzangu kazini wamenisaidia,” anasema.
Anaongeza, “Najaribu kusoma Biblia, na kuomba ninapohisi kuzidiwa, lakini haitoshi.”
Kadri uraibu wa kamari unavyoendelea kuenea miongoni mwa vijana katika mitaa ya mabanda Nairobi, maduka ya kutoa huduma hizi yanaongezeka ishara ya tatizo kubwa zaidi.
Ingawa kamari huanza kama njia rahisi ya kutengeneza pesa, imegeuka kuwa uraibu mbaya usiodhibitika kwa wengi.