Uzalendo kuwa somo linalofunzwa Kenya mswada unaopendekeza ukipitishwa
MAADILI ya kitaifa na kanuni za utawala kama vile uzalendo, umoja wa kitaifa, ugatuzi wa mamlaka na utawala wa sheria zinaweza kuanza kufundishwa shuleni hivi karibuni ikiwa Bunge litaidhinisha Mswada unaopendekezwa kuwa sheria.
Rasimu ya Mswada Marekebisho ya Sheria za Elimu wa 2024 unalenga kurekebisha Sheria mbalimbali za elimu ili kuanzisha sayansi ya taifa kama somo la kutahiniwa kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu kama sehemu ya kuimarisha maadili ya kitaifa kwa wanafunzi mapema maishani.
Mswada huo unaofadhiliwa na Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi unalenga kukuza maadili na kanuni za kitaifa kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 10 cha katiba.
“Lengo kuu la Mswada huu ni kufanyia marekebisho Sheria ya Vyuo Vikuu, 2012, Sheria ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi, 2013, Sheria ya Elimu ya Msingi, 2013 na Taasisi ya Ukuzaji Mtaala ya Kenya, 2013,” unasema Mswada huo.
Kwa mujibu wa ibara ya 10 ya katiba, misingi ya utawala ni pamoja na uzalendo, umoja wa kitaifa, ugatuzi wa mamlaka, utawala wa sheria na demokrasia.
Pia inajumuisha utu wa binadamu, usawa, haki ya kijamii, ushirikishwaji, haki za binadamu, kutobaguliwa na ulinzi wa waliotengwa.
Zaidi ya hayo, Ibara ya 10 pia inajumuisha utawala bora, uadilifu, uwajibikaji na maendeleo endelevu.
Akitetea Mswada huo mbele ya kamati ya Bajeti na Matumizi, Bw Omondi alisema nchi kama vile Singapore na Uswizi ambazo zimejumuisha masomo kama hayo katika mtaala wao zina kiwango cha chini cha ufisadi, zina uwiano zaidi, na zina maendeleo ya juu kiuchumi.
“Pendekezo linalenga kuinua maadili na kanuni hizi kuwa mtaala ambao utafunzwa katika viwango mbalimbali vya mfumo wetu wa elimu. Ukiangalia mashirika yote, nchi ambazo hazina elimu ya aina hii zina matatizo mengi. Hili ndilo litakalofanikisha vita vyetu dhidi ya ufisadi, vita vyetu dhidi ya ukabila, vita vyetu dhidi ya usimamizi mbovu wa kiuchumi, na kimsingi kuunda taifa moja lililojengwa juu ya maadili haya,” Bw Omondi alisema.
Alisema utekelezaji wa pendekezo hilo hautakuwa ghali kwa walipa ushuru akisema faida zinazidi gharama.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA