Vifo vya kutisha vyaendelea kuripotiwa ndani ya seli za polisi
VIFO vya Wakenya ndani ya vituo vya polisi havikomi kwani vimeendelea kutokea kila kuchao katika hali ya kuhofisha, miezi miwili tu tangu nchi hii ifunikwe na ghadhabu kutokana na mauti ya bloga Albert Ojwang’ aliyeaga dunia ndani ya kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi.
Visa vya majuzi vimetokea ndani ya vituo vya polisi katika eneo la Navakholo, Kaunti ya Kakamega na Kaunti ya Murang’a katika kipindi cha siku tano. Mauti ya Navakholo yalitokea Jumapili.
Haya yanajiri huku zaidi ya Wakenya 20 wakiripotiwa kuaga dunia ndani ya seli za polisi kwa siku 15 kati ya Juni 6 na Juni 23, 2025 na kutikisa nchi kupitia maandamano makubwa.
Maafisa wa usalama wamelaumiwa kwa vifo hivyo.
Kwenye kisa cha Kakamega, familia moja imetoa wito kwa Tume Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA) iingilie kati baada ya mwanao kufa ndani ya seli, muda mchache baada ya kunyakwa na polisi mnamo wikendi.
Raymond Nachibati, 33 alinyakwa Jumamosi mchana pamoja na watu wengine wawili baada ya kupigana katika soko la Malaha, Navakholo.
Siku hiyo hiyo mwili wake ulipatikana umenin’inia ndani ya seli ya kituo cha polisi cha Nang’anda.
Mwili wake huo kwa sasa unaendelea kuhifadhiwa katika makafani ya Hospitali ya Kaunti ya Kakamega.
Katika kisa cha Murang’a, kitendawili hakijateguliwa jinsi mwanaume aliyekuwa ameva nadhifu alivyoingia katika kituo cha polisi cha Kenol mnamo Agosti 5 na kujitia kitanzi.
Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini Charity Karimi alisema uchunguzi unaendelea hasa kuhusu madai kuwa mauaji hayo huenda yalitokea katika kituo cha polisi.
Tukio hili linajiri miezi mitano tu baada ya mwanaume mwingine kufia ndani ya kituo cha polisi cha Kiria-ini, Murang’a.
Charles Gathungu 53, alinaswa na kutiwa mbaroni na maafisa wa Kiria-ini akiwa ndani ya baa na mpenzi wake wa kike, na masaa machache baadaye ikasemekana kuwa alijinyonga katika seli.
Bw Gathungu alikamatwa kwa kisingizio kwamba alikuwa na ushirika wa kimapenzi na msichana wa tajiri fulani.
Taarifa ya polisi kuhusu tukio hilo zilidai kwamba Bw Gathungu aliwekwa kwa seli mwendo wa saa tisa mchana lakini akajinyonga kwa kutumia shati lake.
Mkewe maremu, Bi Milkah Wambui, 42, aliteta kwamba hakuna sheria inayowazuia watu wawili wazima wa jinsia tofauti kuwa wapenzi.
“Mimi nilikuwa na ufahamu kuhusu mapenzi hayo ya bwanangu na huyo mwanamke. Kuna makosa gani? Polisi walinipigia simu wakisema bwanangu alikuwa mgonjwa sana na alikuwa amekimbizwa hospitalini Kiria-ini,” Bi Wambui asema.
Katika matukio yaliyofuata, wasimamizi wa hospitali hiyo walikana kumpokea Bw Gathungu kama mgonjwa wa kutibiwa lakini kama maiti aliyeletwa kwa gari la polisi.
Hadi leo, familia ya Bw Gathungu haijapata haki na Bi Wambui anasema kwamba “mimi na unyonge wangu nilimwachia Mungu”.
Kuhusu kisa cha Kakamega mnamo Jumamosi, Kamanda wa Polisi wa Kaunti-ndogo ya Navakholo, Mohammed Hassan alisema marehemu alijitia kitanzi ndani ya kituo cha polisi akitumia jaketi yake.
“Mshukiwa anayetambuliwa kama Raymond alinyakwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Budonga. Kwa masikitiko makuu alitumia kamba ya jaketi yake kujitia kitanzi na alionekana mwenye msongo wa mawazo akiwa amelewa.
Hatukufikiria kuwa angefikia mahali ambapo angejitoa uhai,” akasema Bw Hassan.
Alisema maafisa kutoka Idara ya Upelelezi (DCI) wanashirikiana na wenzao wa IPOA kuendesha uchunguzi kuhusu mauti hayo.
“Alifikishwa kituoni humo saa tisa lakini akapatikana ameaga dunia ndani ya muda wa saa mbili. Uchunguzi unaendelea eneo la tukio,” akasema Bw Hassan.
Kwa mujibu wa polisi, Nachibati alikamatwa akipigana na mkewe sokoni kisha akapelekwa kwenye kituo hicho kidogo kabla ya uchunguzi kuanza.
Ndugu zake wawili Sylvanus Waswa na Ibrahim Barasa walioenda kituo cha polisi kufahamu kwa nini alinyakwa, wakitaka aachiliwe, walisema walishangazwa walipouona mwili wa ndugu yao ukining’inia kwenye paa la seli.
“Alikamatwa pamoja na mkewe na ndugu yake mkewe kwa kupigana sokoni . Wawili hao hawakuwa kwenye seli na mwili wa ndugu yetu ulikuwa ukining’inia katika seli, hapa tunashuku kitu,” akasema Bw Waswa. Familia yake imesema haitaendelea na mazishi hadi polisi wawaeleze kilichosababisha mwanao kufa.
Babake Anderson Makokha aliuliza kwa nini mwanawe aliachwa pekee kwenye seli ilhali alikamatwa na watu wengine wawili. Pia anataka kujua kulikotoka kamba aliyotumia kujitia kitanzi.
“Nilishutuka nilipoambiwa mwanangu Nachibati amekamatwa kwa kupigana na mkewe. Hili ni jambo ambalo tungelitatua nyumbani,” akasema Bw Makokha.
Mama Esther Khaemba mamake marehemu alisema Nachibati alipigana na mke waliyetengana naye. Mke huyo alikuwa amezua maswali kuhusu Nachibati kumwoa mke mwingine.
Kwa mujibu wa jamaa mwingine wa familia, Nachibati alikuwa ametengana na mkewe na kumwoa mwingine siku mbili zilizopita kabla ya Jumamosi.
“Alipogundua mwanangu alikuwa ameoa tena, alirejea na kuanzisha vita. Mwanangu aliingilia kati na kumfukuza hadi sokoni lakini akavamiwa na ndugu zake ndipo maafisa wa polisi wakawakamata watatu hao na kuwapeleka kituo cha polisi cha Budonga,” akasema.