Vijana zaidi wa Gen Z kushtakiwa kwa ugaidi kwa kuandamana Saba Saba
SERIKALI itawafungulia mashtaka yanayohusiana na ugaidi vijana saba waliokamatwa Kaunti ya Machakos wakati wa maandamano ya Saba Saba mwanzoni mwa mwezi huu, huku Mbunge wa Manyatta, John Mukunji, akishtaki serikali mahakamani akitaka isitumie Sheria ya Kuizuia Ugaidi kunyamazisha wakosoaji.
Vijana hao sita, wanne wa kiume na mmoja wa kike, walikamatwa tena juzi huko Kithimani, Machakos, baada ya mashtaka ya kuchoma moto na uharibifu wa mali yaliyowakabili kuondolewa.
Saba hao wanatarajiwa kufikishwa mbele ya Mahakama ya Kahawa Jumatano asubuhi, na kujiunga na orodha inayoendelea kuongezeka ya watu wanaofunguliwa mashtaka ya ugaidi kufuatia maandamano ya Juni 26 na Julai 7.
Wengine kumi kutoka Matuu, Machakos tayari wanakabiliwa na mashtaka kama hayo, kufuatia maandamano ya Juni 26.
Katika Mahakama ya Kahawa, Hakimu Mkuu Mwandamizi Richard Koech alikataa maombi ya upande wa mashtaka ya kuwanyima dhamana watu wanne waliohusishwa na shambulio la kuchoma Kituo cha Polisi cha Mawego, Kaunti ya Homa Bay, Julai 3.
Kennedy Oluoch, Nicholas Otieno, Tofiq Owiti Mohamed, Michael Omondi Opiyo, David Bill Clinton Otieno, Robert Ouko Abala, Samuel Ouma Odhiambo na Erick Obunga Osumba walikanusha mashtaka matatu ya kuhusika na kitendo cha ugaidi, kuchoma moto na kuharibu mali.
Hakimu Koech alisema upande wa mashtaka haukutoa sababu za kutosha za kuwanyima dhamana.
Katika Mahakama Kuu, Bw Mukunji, ambaye alikamatwa Julai 7 wakati wa maandamano ya Saba Saba pamoja na mwandishi wa habari James Ikuwa na Stanley Mbuthia, alisema kuna mwelekeo unaoibuka na wa kusikitisha wa kushtaki waliohusika na maandamano na mashtaka chini ya Sheria ya Kuizuia Ugaidi.
Alisema Sheria hiyo, iliyopitishwa kufuatia mashambulishi ya kigaidi nchini, haikunuiwa kutumiwa kuwadhibiti watu wanaopinga serikali.
Bw Mukunji na washukiwa wawili wako nje kwa dhamana baada ya mahakama ya Kahawa kukataa maombi ya upande wa mashtaka kuwazuia kukamilisha uchunguzi.