Habari za Kitaifa

Viongozi kutoka Meru wakataa mwaliko wa Ruto Ikulu wakilalama miradi imekwama

Na GITONGA MARETE NA DAVID MUCHUI May 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MKUTANO ulioitishwa Jumatano, Aprili 30, 2025 katika Ikulu ya Nairobi ambapo Rais William Ruto angekutana na viongozi kutoka Kaunti ya Meru uliahirishwa dakika za mwisho kutokana na malalamishi kuhusu miradi iliyokwama.

Badala yake, baadhi ya viongozi walikutana na Rais Ruto Jumanne (Aprili 29) na kuelezea kutoridhishwa kwao na miradi hiyo, hali inayodaiwa kuwa chanzo cha mvutano kati ya utawala wa Kenya Kwanza na viongozi wa Meru.

Mwakilishi wa Wadi (MCA) mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema mkutano ambao ungeleta pamoja viongozi zaidi ya 500 uliahirishwa ili kuruhusu kukamilishwa kwa miradi.

“Kuna kelele nyingi kwa sasa kuhusu miradi na ilikubaliwa kuwa rais atakutana na viongozi wote mara tu itakapotekelezwa,” alisema mwakilishi huyo.

Seneta Kathuri Murungi alisema katika mkutano wa Jumanne, walijadili masuala muhimu yanayoathiri eneo hilo ikiwemo barabara zilizokwama, pamoja na mapato ya wakulima wa majani chai, kahawa, miraa, maziwa, na parachichi.

Gavana wa Meru, Isaac Mutuma, aliwaongoza wabunge na madiwani kuwasilisha malalamishi yao.

Umaarufu wa Rais Ruto katika eneo la Mlima Kenya Mashariki umepungua kufuatia kuondoka kwa waliokuwa washirika wake serikalini wakiwemo aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na aliyekuwa Waziri wa Huduma za Umma Justin Muturi.

Meru, kumekuwa na kilio kuhusu mashambulizi ya wizi wa mifugo ambayo yamesababisha vifo vya watu 20 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Rais Ruto, pia, anakabiliana na upinzani kuhusu kushuka kwa bei ya miraa kutokana na mtandao wa watu wenye ushawishi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akizungumza katika mahojiano na Weru TV ya Meru Jumapili iliyopita, alidai kuwa serikali inalinda mtandao huo.

Mbunge wa Igembe Kusini, John Paul Mwirigi, alisema walijadili miradi iliyokwama na inayotekelezwa, usalama, na juhudi za serikali kuimarisha uchumi.

Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kaunti ya Meru, Jim Muchui, alisema rais alisisitiza ahadi yake ya kukamilisha miradi iliyokwama na mipya katika kaunti.

Alisema Rais Ruto pia aliahidi kuwa serikali kuu italipa deni la Sh329 milioni ambalo kaunti inadaiwa na mjasiriamali wa Kifaransa aliyefukuzwa kutoka Hifadhi ya Kitaifa ya Meru.

Rais Ruto aliwataka viongozi wa Meru kuungana na kuepuka siasa za migawanyiko, akisema ataunda mazingira bora ya maendeleo kwa serikali zote za kaunti na kitaifa.

Mkutano huo ulifanyika siku chache baada ya Bw Linturi kujiunga na upinzani akiahidi kushawishi wakazi kumng’oa Rais Ruto.

Mabw Linturi na Muturi, Jumanne walijiunga na kambi ya Gachagua, Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Fred Matiang’i na Eugene Wamalwa katika juhudi za kusuka muungano wa kumshinda Rais Ruto.

Katika kaunti ya Meru, rais sasa ana wapinzani ambao ni; Linturi, aliyekuwa gavana Kawira Mwangaza na aliyekuwa waziri Peter Munya.