Viongozi wa kidini waungane kurudisha nidhamu na maadili katika jamii
NI WAZI kuwa nidhamu imedorora katika jamii na iwapo hali hii itaendelea, nchi itakuwa pabaya.
Ili kurekebisha hali hii, ni lazima viongozi ambao wanachangia pakubwa uozo uliopo kwa vitendo, matamshi na misimamo yao wawe mstari wa mbele kuchukua hatua za kimakusudi kama wanavyofanya maaskofu wa kanisa la Kiangilikana na Katoliki Kenya.
Hatua ya maaskofu hao kuzima wanasiasa kuhutubu makanisani inanuiwa kurejesha nidhamu katika maabadi.
Hii ni baada ya wanasiasa kutumia vibaya heshima waliyopewa kwa kuruhusiwa kuwasalimu waumini kuzungumzia siasa na kuwashambulia wapinzani wao, kuonyesha kiburi na kuzua migawanyiko miongoni mwa waumini na Wakenya kwa jumla.
Kwa kuwa viongozi wa kidini wana jukumu na ushawishi mkubwa katika jamii, wakiungana kimakusudi wanaweza kurudisha nidhamu na maadili katika jamii yetu kwa kubuni mwongozo na kuuzingatia kikamilifu sio tu kuzima wanasiasa bali pia kwa kushauri jamii na hasa vijana ambao huiga viongozi wa kisiasa na kidini.
Hii inawezekana kupitia mashirika ya kitaifa ya makanisa na dini tofauti.
Iwapo viongozi wa kisiasa wanaoendelea kukashifu hatua ya kuzimwa kwao kuhutubu katika baadhi ya makanisa wangekuwa wanajali, wangebadilisha tabia na kuunga juhudi kama hizi kwa lengo la kuokoa kizazi cha sasa na vijavyo.
Hata hivyo, matamshi na vitendo vya wanasiasa hao vinavyochangia kudorora kwa maadili na nidhamu hunuiwa kuendeleza ajenda za kisiasa na kwa kufanya hivi kusababisha uozo wa kimaadili katika jamii.
Hii ndiyo sababu viongozi wa kidini wanafaa kuungana na kuwa na azma moja ya kurejesha maadili na nidhamu katika jamii bila kuyumbishwa na wanasiasa.