Viongozi wa Mlima wajitenga na kauli za Kahiga za ‘kufurahia’ kifo cha Raila
VIONGOZI kutoka eneo la Mlima Kenya na magavana nchini, wamejitenga na kauli za gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga anazoonekana kusherehekea kufariki kwa aliyekuwa waziri mkuu hayati Raila Odinga.
Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambaye pia ni Gavana wa Embu Cecily Mbarire amemkosoa vikali Kahiga kwa kauli aliyoitoa kufuatia kifo cha Raila, akisema kuwa ni kauli “zisizo za busara na zisizo na huruma.”
Katika taarifa aliyotoa Alhamisi, Oktoba 21, 2025, Mbarire alisema kauli za Kahiga zimemkera sana, kwa kuwa zilionekana kuonyesha kwamba kifo cha Raila ni kwa nguvu za kiungu kwa manufaa ya mipango ya kisiasa ya eneo la Mlima Kenya.
Akizungumza katika mazishi yaliyofanyika Nyeri, Kahiga, akizungumza kwa Kikuyu, aliwaambia waombolezaji kuwa “Mungu ameingilia kati” kwa ajili ya Mlima Kenya, akieleza kwamba uhusiano wa karibu wa Raila na Rais William Ruto uligeuza rasilmali za serikali kuelekea Nyanza.
Bi Mbarire aliwatenga viongozi wa eneo la Mlima Kenya na chama tawala na kauli hizo, akisisitiza kuwa maneno ya Kahiga hayawakilishi maoni au misimamo ya viongozi wa eneo hilo.
“Wakati huu taifa letu linapohuzunika, kauli kama hizi ni dharau kubwa, kwa kumbukumbu ya kiongozi mkuu na pia kwa mamilioni ya Wakenya wanaohuzunika kwa kumpoteza,” alisema.
Alimpongeza Raila akimtaja kama“shujaa wa kweli wa ugatuzi, aliyeamini katika kuwezesha kaunti na kuimarisha utawala,” na kuongeza kuwa urithi wake unastahili kuheshimiwa, sio kudhalilishwa.
“Ieleweke wazi: Maneno ya Gavana Kahiga hayawakilishi maoni ya eneo la Mlima Kenya. Baba alikuwa shujaa wa kweli wa ugatuzi, aliyeamini katika kuwezesha kaunti na kuimarisha utawala. Katika hili, tuko pamoja,” alisema.
Mbarire aliitaka serikali ya Kahiga kuomba msamaha na kuwataka viongozi wa vyama vyote kuondoa migawanyiko midogo na kuhimiza umoja wa kitaifa wakati huu wa huzuni..
Chama cha ODM kimemkosoa vikali Gavana Kahiga kwa kauli zake zinazodai kuwa kifo cha Raila Odinga ni “mkono wa kiungu.”
Naibu Kiongozi wa ODM Abdulswamad Sheriff Nassir, katika taarifa yenye maneno makali, alikosoa kauli za Kahiga akisema hazina busara, za kugawanya na za aibu, akisema zimedhalilisha kumbukumbu ya kiongozi huyo wakati huu wa huzuni.
“Katika wakati ambapo mamilioni ya Wakenya kutoka makabila, dini na mirengo mbali mbali ya siasa bado wanahuzunika, Gavana Kahiga alichagua kuongeza chumvi katika majeraha ya taifa,” Nassir alisema.
Aliongeza kuwa maisha ya Raila Odinga yalionyesha “umoja wa kitaifa, ujumuishaji na maridhiano,” na maneno ya Kahiga hayawakilishi “chochote kile ambacho taifa letu linapaswa kuendelea nacho.”
“Licha ya maneno haya yasiyofaa, tunaendelea kushikilia thamani ya umoja na ujenzi wa taifa. Tutaendelea kufanya kazi kwa nia njema kuelekea Kenya yenye mshikamano, haki na ustawi,” Nassir alisema.
Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru amemkosoa Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga kwa kusherehekea kifo cha Raila Odinga.
Katika chapisho katika mitandao ya kijamii Jumanne, Oktoba 21, 2025, Waiguru alisema maneno ya Kahiga ni ya aibu, yasiyo na huruma na yasiyokuwa na uwajibikaji.
Waiguru alisema kauli za Kahiga hazihusiani na maoni ya viongozi au watu wa Mlima Kenya.
“Maneno yaliyotolewa leo na gavana mwenzangu, Gavana wa Nyeri Kahiga, si tu ya aibu bali hayana huruma na yasiyo na uwajibikaji. Hayawakilishi maoni ya viongozi wala watu wa Mlima Kenya. Tuwe wazi: siasa haziondoi heshima ya msingi. Sisi kama watu, tuko pamoja na Kenya yote katika kuomboleza kiongozi mkuu, Raila Odinga, CGH,” Waiguru alisema.