Waasi wa ODM: Nafikiri mmeona sasa kwa nini tulitangulia mapema kwa Ruto!
BAADHI ya viongozi waliochaguliwa kutoka Nyanza ambao waliitwa ‘waasi’ kwa kushirikiana na Rais William Ruto wanasema wameondolewa lawama baada ya wakosoaji wao kuteuliwa katika baraza la mawaziri.
Wanasema walikuwa na maono katika hatua yao ya kijasiri waliyochukua mapema ya kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza.
Viongozi hao walisema licha ya kutukanwa na wafuasi wa upinzani waliowaita wasaliti, kwa sasa ni wazi kuwa wapinzani umebaini ni lazima ushirikiane kwa karibu na serikali ili kuhakikisha nchi ni tulivu.
Kauli zao zilijiri siku chache baada ya washirika wa kiongozi wa ODM Raila Odinga ambao ni viongozi wakuu wa ODM kuteuliwa katika baraza la mawaziri la serikali ya Rais Ruto.
Wanne hao ni Mwenyekiti wa National Orange Democratic Movement Party na mbunge mteule Bw John Mbadi (Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Kiuchumi), Naibu Viongozi wa Chama cha ODM Hassan Joho (Madini, Uchumi wa Baharini na Masuala ya Bahari) na Wycliffe Oparanya (Ushirika na Biashara Ndogo) na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi (Nishati na Petroli).
Wanne hao wamekuwa msitari wa mbele kuwakosoa ‘waasi’ kwa kushirikiana na Rais Ruto na kutumia mifumo ya chama kutishia kuwaadhibu.
Mnamo Februari, mwaka jana, viongozi hao walikutana na Rais Ruto Ikulu, Nairobi kinyume na msimamo wa Bw Odinga.
Waliozuru Ikulu ni pamoja na Mbunge wa Kisumu Mashariki Shakeel Shabbir ambaye alichaguliwa kuwa mgombeaji huru, Seneta wa Kisumu wa ODM Tom Ojienda na wabunge wa Bunge la Kitaifa Bw Mark Nyamita (Uriri), Elisha Odhiambo (Gem), Dkt Gideon Ochanda ( Bondo), Paul Abuor (Rongo), Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o (Langata) na Caroli Omondi (Suba Kusini).
Baadaye walitimuliwa kutoka kwa kamati na kukabiliwa na hatua za kinidhamu kutoka ODM ambacho kilianzisha mchakato wa kuwaondoa chamani na kushinikiza wajiuzulu kwao kama wabunge.
“Tulishutumiwa na kuitwa majina lakini sasa nafurahi kwamba tumeondolewa lawama. Kulikuwa na mvutano wa kisiasa kati ya ODM na muungano wa Kenya Kwanza na tulikuwa wa kwanza kuona umuhimu wa kufanya kazi na serikali mapema kwa manufaa ya watu wetu. Nimefurahi kwamba waliokuwa wakitukosoa, wamejiunga nasi,” akasema Seneta Ojienda.
Dkt Ochanda anasema hajuti kuchakua hatua ya kijasiri.
“Baada ya uchaguzi, baadhi ya watu walikuwa bado na mashaka kwamba tuna Serikali, tulichukua hatua ya kijasiri ya kuitambua Serikali iliyopo madarakani, tulienda na kama Ojienda na sasa waliotuhukumu wamezunguka huku na kule lakini wameishia kuwa pamoja nasi,” alisema Dk Ochanda.
Bw Nyamita alitaja uteuzi huo kuwa mzuri na kuwataka Wakenya kukumbatia mazungumzo.
Bw Nyamita alifurahi kwamba Rais Ruto ameondoa uadui wa kisiasa na kuungana na wanaodhaniwa kuwa wapinzani wake wa kisiasa.