Wabunge kurejea kutoka likizo Jumanne, siku ambayo maandamano mengine yamepangwa
WABUNGE wanarejelea vikao vya kawaida kesho Jumanne baada ya likizo ya mwezi mmoja siku ambayo maandamano ya kupinga serikali yamepangiwa kufanyika kote nchini.
Wabunge wanarejelea shughuli rasmi wakati ambapo Wakenya wanaonekana kupoteza imani nao huku wakitarajiwa kuwapiga msasa watu 11 waliopendekezwa na Rais William Ruto kushikilia nyadhifa za uwaziri.
Mojawapo ya sababu ya kuitishwa kwa maandamano hayo ni kwa mawaziri sita waliofutwa kazi na Rais Ruto mnamo Julai 11, 2024.
Wao ni Kithure Kindiki (Usalama), Bi Alice Wahome (Ardhi) Aden Duale (Ulinzi ), Davis Chirchir (Barabara), Soipan Tuya (Mazingira) na waziri wa zamani wa Biashara Bi Rebecca Miano ambaye amependekezwa kuwa Mwanasheria Mkuu.
Wabunge pia watashughulikia Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ugavi wa Mapato ya 2024, Mswada wa Kuhusu Utengaji wa Fedha katika Kaunti ya 2024 na kuidhinishwa na watu waliopendekezwa kuhudumu katika jopo la kuteua Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Aidha, wabunge watajadili Bajeti ya Ziada ya Kwanza katika Mwaka wa Kifedha wa 2024/2025 na ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Fedha kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024.
Isitoshe, wabunge pia watashughulikia upya sheria kadhaa kuhusu Afya—Sheria ya Afya ya Kimsingi ya 2023, Sheria ya Afya ya Kidijitali ya 2023 na Sheria ya Bima ya Afya ya Kijamii ya 2023.
Hii ni baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa kusitisha utekelezaji wa sheria hizo kwa misingi kuwa zilipitishwa pasina kushirikishwa kwa maoni kutoka kwa umma na hivyo ni batili kikatiba.
Hata hivyo, mahakama hiyo iliipa Bunge siku 120 kurekebisha sheria hizo ili ziafiki matakwa ya Katiba.
Ratiba ya wabunge pia inaonyesha kuwa wabunge kwa ushirikiano na maseneta watampiga msasa Dkt Patrick Amoth ambaye amependekezwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Afya.
Dkt Amoth, ambaye ameshikilia wadhifa huo kama kaimu tangu 2019, alipendekezwa na aliyekuwa Waziri wa Afya Susan Nakhumicha mnamo Juni 26, 2024
Wabunge wanarejelea vikao baada ya majengo ya bunge kuharibiwa na waandamanaji waliyoyavamia mnamo Juni 25, 2024 wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z.
Hii ni baada ya vijana hao kukasirishwa na hatua ya wabunge kupitisha Mswada wa Fedha wa 2024. Inasemekana kuwa mali ya thamani ya Sh350 milioni iliharibiwa wakati wa maandamano hayo.
Sehemu zilizoharibiwa zaidi na afisi za uongozi wa bunge, kitengo cha usalama, ua, eneo la mankuli, eneo ambako wabunge hupumzika na afisi za wafanyakazi.
“Hatua kubwa imepigwa katika ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa. Ukumbi wa mijadala pia umefanyiwa ukarabati na sasa ni tayari kwa matumizi,” afisa mmoja, aliyeomba tusimtaje jina, akasema.