Wabunge vijana waunda vuguvugu wanalosema litamfanya Ruto ‘WanTam’
BAADHI ya viongozi chipukizi wameanzisha vuguvugu wanalosema litakomboa nchi huku wakiapa kuendeleza kampeni kali za kumpleka Rais William Ruto nyumbani katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Jana, viongozi hao ambao wabunge vijana kutoka mirengo yote ya kisiasa, walizindua vuvugu linalofahamika kama ‘Kenya Moja’ ambalo walisema litapinga Serikali Jumuishi, ‘Broad Based Government’.
Wabunge hao wakiwa kwenye eneobunge la Saboti Kaunti ya Trans Nzoia, walisema kuwa lengo lao ni kuhakikisha kuwa utawala wa sasa unaenda nyumbani na Wakenya wanapata uongozi bora.
Waliapa kuwa watawapuuza vinara wa kisiasa nchini na kuzungumza kwa lugha moja ya kuwatetea Wakenya wanaoendelea kunyanyaswa na uchumi mgumu.
Wabunge hao waliongozwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, mwenyeji wao Caleb Amisi, Gathoni wa Muchomba (Githunguri), Babu Owino (Embakasi Mashariki), Majimbo Kalasinga (Kabuchai), Clive Gisairo (Kitutu Masaba), Jack Wamboka (Bumula) na Joshua Kimilu (Kaiti).
Walikuwa wakishiriki michango ya kuinua akina mama kwenye eneobunge la Saboti, Kaunti ya Trans Nzoia.
Bw Sifuna ambaye alichangisha jumla ya Sh1 milioni wakati wa hafla hiyo iliyoitwa Kikao na Mama Mboga, alisema ataendelea kukosoa serikali ya sasa wala hatishwi na wito wa baadhi ya viongozi kuwa atafurushwa ODM.
“Nashikilia msimamo wangu na nataka kuwaambia wale mabroka ODM kuwa nina haki ya kutoa maoni yangu. Nitakuwa nasoma maafikiano ya chama isipokuwa yale ambayo chama kitasema kuwa kitamuunga Rais Ruto mnamo 2027,” akasema Bw Sifuna.
Seneta huyo alisema kuwa hana kinyongo cha kibinafsi na Rais ila kuondolewa kwake afisini mnamo 2027 ni jambo linalozingatia maslahi ya taifa.
“Hii si chuki ya kibinafsi lakini kama viongozi ambao wanasimamia uongozi bora na haki, hatuwezi kuruhusu utawala huu uendelee kuwanyanyasa Wakenya,” akaongeza Bw Sifuna.
Wabunge hao walisema Kenya Moja ni vuguvugu la wabunge chipukizi ambao wanaolenga kuwaokoa Wakenya kutoka dhuluma ya utawala wa Kenya Kwanza.
Bw Sifuna alisema yuko tayari kwa mazungumzo na viongozi wengine akiwemo Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya mradi tu wampeleke nyumbani Rais Ruto mnamo 2027.
“Niko tayari kuondolewa kama katibu wa ODM kwa sababu nimeambiwa kuna mtu ambaye ameidhinishwa achukue nafasi yangu,” akasema Bw Sifuna.
Bw Amisi alisema kuwa mkutano huo ulikuwa mwanzo wa mikutano mingine mingi watakayoiandaa kote nchini kuhakikisha kuwa kama viongozi vijana, wanakomboa Kenya.
“Sisi tunawainua makundi ya vijana na wanawake kutoka uchumi huu mgumu wala hatushiriki ubabe na ile hafla inayoandaliwa na Kenya Kwanza,” akasema Bw Amisi ambaye pia ni mbunge wa ODM.
Bw Amisi alidai amekuwa akiandamwa na vikosi vya usalama na alidai wiki jana alinusurika jaribio la kumuua Nairobi lakini hilo halifanya atetereke.
“Huwezi kutuua sote na maovu unayotutendea yanafanya tu tuendelee kupigania haki,” akaongeza Bw Amisi akisema yuko tayari kuondoka ODM iwapo chama hicho kitaunga kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto 2027.
Bw Majimbo alisema kuwa wanaunganishwa na hali kwamba wao ni viongozi vijana na wanapigania mabadiliko ya uongozi nchini.
“Hatuwezi kuketi tu na kuona taifa letu likielekea pabaya. Tunashinikiza kuwa na nchi ambapo kila Mkenya amefurahi badala ya mateso wanayoyapitia kwa sasa,” akasema Bw Majimbo ambaye ni kati ya viongozi waasi wa Ford Kenya.
Bw Oundo naye aliwaonya polisi dhidi ya kuendelea kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya Wakenya wanaopigania haki zao.
Bi Wamuchomba alidai kuwa sekta ya ya elimu na afya imeporomoka chini ya Kenya Kwanza akitaja mpango wa Linda Mama ambao alidai haufanyi tena na kupunguzwa kwa ufadhili kwenye sekta ya elimu.
“Nilimwaambia Rais akome kusema uongo na kusimamia nchi vibaya. Ningekuwa yeye ningewasikiza Wakenya. Nitasimama upande unaopigania haki na maslahi ya Wakenya badala ya kuunga serikali ambayo inawadhulumu raia wake,” akasema Bi Wamuchomba.