Wabunge wataka miradi iwekwe kwenye bajeti kuzima ahadi hewa
VIONGOZI kutoka Magharibi wanasukuma sana ili miradi ambayo Rais William Ruto aliahidi kwenye ziara zake za awali, itengewe fedha kwenye bajeti ya 2025/2026.
Wabunge hao walikutana na Rais Ruto kwenye Ikulu ya Nairobi mnamo Jumatano, Machi 26, 2025 ambapo walimuomba kiongozi wa nchi kuwa miradi hiyo itengewe pesa.
“Mnajua ahadi ambazo zinatolewa na rais huwa ni semi tu za barabarani anapozuru maeneo mbalimbali. Miradi hiyo itakuwa na maana tu iwapo itatengewa pesa katika bajeti na kutekelezwa,” akasema mbunge mmoja ambaye alikuwa Ikulu na hakutaka jina lake linukuliwe.
Hatua ya wabunge kutaka miradi hiyo itengewe fedha imekuja kwa wakati kwa sababu mchakato wa kuandaa bajeti ya 2025/26 bado unaendelea.
“Tulimwaambia Rais kuwa tunataka pesa zitengewe miradi ambayo aliahidi ili tusisalie gizani na kukumbana na ghadhabu za wananchi jinsi ambavyo imefanyika hapo awali alipotoa ahadi,” akasema mbunge mwengine.
Kando na miradi, duru ziliarifu kuwa wabunge wa Ford Kenya walisimama kidete na kusisitiza Waziri Deborah Mulongo hapaswi kufutwa kazi (ingawa angali serikalini) licha ya utendakazi wake ambao haukuwa umewaridhisha Wakenya.
Ombi hili lilionekana kuzaa matunda baada ya Bi Mulongo kuhamishwa hadi wizara ya mazingira kwenye mabadiliko ambayo rais alifanyia baraza lake la mawaziri wiki hii.
Mkutano huo wa Ikulu uliofanyika kati ya saa moja na saa nne asubuhi, ulihudhuriwa na wabunge na magavana wote isipokuwa Wilbur Ottichilo ambaye yupo ziarani nje ya nchi na wabunge Caleb Amisi (Saboti) na Peter Salasya (Mumias Mashariki).
Mkutano huo uliidhinishwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga huku Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi akiwaongoza wabunge wa ODM naye Mbunge wa Tongaren John Chikati akiongoza wale wa Ford Kenya.
Baadhi ya wabunge waliohudhuria walisema Bw Amisi alikataa kuhudhuria mkutano naye mbunge huyo akakanusha madai hayo akisema alifahamu kuhusu mkutano huo mtandaoni.
“Hawakunialika kwa mkutano wa Ikulu,” Bw Amisi akaambia Taifa Leo.
Bw Osotsi hakupokea simu kuzungumzia walichojadili, naye mbunge wa Lugari Nabii Nabwera hakufichua kilichojadiliwa.
“Nathibitisha kuwa nilikuwa mkutanoni lakini si kazi yangu kufichua kilichojadiliwa,” akasema Bw Nabwera, mbunge wa ODM.