Wafanyakazi 108 wa Gachagua watumwa likizo ya lazima
WAFANYAKAZI katika afisi ya Naibu Rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua ndio waathiriwa wa hivi punde wa masaibu yanayomkumba kiongozi huyo baada ya wao kutumwa likizo ya lazima.
Kwenye taarifa Jumamosi serikali iliamuru jumla ya wafanyakazi 108 katika walioajiriwa mahsusi kumhudumia Bw Gachagua kwenda likizo kutokana na kile kinachotajwa kama “mchakato wa kikatiba unaoathiri naibu rais.”
Walioathirika ni pamoja na maafisa wakuu, washauri na makatibu walioajiriwa kwa kandarasi na mkataba wa kudumu.
Taarifa hiyo iliyotumwa na Katibu wa Usimamizi Patrick Mwangi na nakala yake kutumiwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, wengi wa maafisa walioagizwa kuondoka ni wale wa kiwango cha ajira cha T na U.
Wakuu wote wa Idara wameagizwa kuhakikisha agizo hilo limetekelezwa kufikia saa sita adhuhuri Jumamosi, Oktoba 19.
Hatua hiyo ya serikali inaonekana kama inayolenga kutoa nafasi kwa utekelezaji wa mageuzi katika Afisi ya Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki akitarajiwa kushika usukani.
“Wakuu wote wa Idara wanaagizwa kuhakikisha kuwa wameteua, kwa maandishi, afisa atakayesimamia idara zao, na nakala ya barua hizo zitumwe kwa Mkuu wa Wafanyakazi na Katibu Msimamizi,” akasema Bw Mwangi.
Miongoni mwa walioasimamishwa kazi ni aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu ambaye amekuwa akihudumu kama mshauri wa kisiasa wa Bw Gachagua na mbunge wa zamani wa Embakasi Magharibi George Theuri aliyekuwa akihudumu kama mshauri wa kuhusu masuala ya vijana.
Bi Elizabeth Wanjiku, ambaye amekuwa akihudumu katika wadhifa wa Mkuu wa Wafanyakazi katika Afisi ya Naibu Rais pia ni mwathiriwa.
Bw Gachagua aliondolewa mamlakani na Bunge la Kitaifa baada ya wabunge 282 kupitisha hoja iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Bw Mutuse aliwasilisha mashtaka 11 dhidi ya Bw Gachagua, yakiwemo ukiukaji wa Katiba na utovu wa maadili.
Hata hivyo, Bw Gachagua alikana mashtaka hayo yote na kuwasilisha kesi ya kupinga kuondolewa kwake afisini.
Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita ametoa agizo la kusitishwa kwa muda kwa mpango wa kumwapisha Profesa Kindiki hadi Oktoba 24 wakati kesi iliyowasilishwa na Gachagua itakapotajwa mbele ya majaji watatu watakaoteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Aidha, duru zinasema kuwa wafanyakazi wote wa serikali waliokuwa wakihudumu katika boma la Bw Gachagua, Mathira, Nyeri, waliagizwa waondoke Ijumaa asubuhi.
Hatua hiyo ilijiri saa chache baada ya Seneti kuidhinisha hatua ya Bunge la Kitaifa ya kumwondoa afisini, Alhamisi usiku.
Wafanyakazi hao ni pamoja na wapishi na maafisa wa usalama waliokuwa wakilinda boma lake.
Waliagizwa kuondoka mnamo Ijumaa saa kumi na mbili alfajiri.
Magari rasmi ya Bw Gachagua pia yaliondolewa.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga