Habari za Kitaifa

Wagonjwa wazidi kuhangaika mfumo wa SHIF ulionunuliwa Sh104 bilioni ukikwama

Na LEON LIDIGU October 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAMIA ya wagonjwa kote nchini wanaendelea kuhangaika mfumo mpya wa Afya ya Huduma ya Jamii (SHIF) ukifeli.

Baadhi ya hospitali sasa zimerejea mfumo wa zamani wa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) ili kushughulikia wagonjwa.

Hii ni baada ya Mfumo wa Teknolojia ya Habari ya Huduma ya Afya (IHTS) ambao ulinunuliwa na serikali kutoka kwa kampuni ya Safaricom kwa Sh104.8 bilioni kufeli.

Uharibifu huu wa kiteknolojia umalazimu hospitali kurejea mfumo wa zamani wa NHIF jambo ambalo linachelewesha mchakato wa kutoa huduma hospitalini.

Wataalam wa ICT katika Shirika la Afya ya Dijitali (DHA) waliopewa jukumu la kutekeleza mfumo mpya wa SHIF walikiri kwamba bado wanajaribu kujifunza ili kuuelewa mfumo huo wenyewe na wanahitaji muda kuuelewa kikamilifu.

“Kumbuka huu ni mfumo mpya ambao serikali ilinunua. Sio eti sisi ndio tumeuunda. Bado tunajaribu kusoma vipengele vya mfumo ambao ulinunuliwa na wizara ya afya ili tuelewe kabisa kabla ya kutoa mafunzo kwa wahudumu wa hospitali kote nchini jinsi ya kuutumia na hivyo basi kuna uwezekano wa kutokea matatizo,” afisa mkuu afisa katika DHA, alisema.

Afisa huyo pia alisisitiza kwamba changamoto za kiteknolojia ambazo zinakumba mfumo huo mpya zimefanya iwe vigumu kwa vituo vya afya kushughulikia na kutatua matatizo ya wagonjwa na kwamba sehemu ya mfumo wa kibayometriki pia bado ni shida kubwa.

Vituo vingi vya afya vya umma na vya kibinafsi kaunti za Kakamega, Nairobi, Eldoret, Mombasa, Kiambu, Machakos, Murang’a na Mandera vinatatizika na mifumo hiyo jambo ambalo limewaathiri wagonjwa mno.

“Mfumo wa NHIF ni rahisi zaidi kutumia ikilinganishwa na la SHA,” msimamizi wa hospitali moja kaunti ya Kiambu aliambia Taifa Leo.

Afisa Mkuu Mtendaji mwingine wa hospitali ya rufaa alikiri kuwa mfumo huo mpya una changamoto ambazo zimewalazimisha kushughulikia wagonjwa kwa kutumia NHIF.

Alipopigiwa simu kuhusiana na matatizo hayo, Katibu wa Huduma za Matibabu Harry Kimtai alisema, “Sijui, nenda ukaulize Safaricom.”

Mnamo Septemba 25, 2024, kamati ya idara ya Afya ikiongozwa na Mbunge wa Endebess, Dkt Robert Pukose iliwataka maafisa wa Wizara ya Afya kujitetea baada ya mfumo huo mpya kufeli wakati wa majaribio yaliyofanywa katika kaunti za Marsabit na Tharaka Nithi.

Wiki iliyopita, kaimu Mkurugenzi Mkuu wa SHA, Bw Elijah Wachira aliwaomba msamaha Wakenya baada ya mfumo huo kufeli na kuacha maelfu ya wagonjwa kote nchini wakiwa wamekwama.