Habari za Kitaifa

Waititu asotea jela

Na SIMON CIURI March 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu amefunguka na kusimulia madhila anayopitia gereza la Nairobi, maisha ambayo ni tofauti kwa kiongozi aliyezoea mamlaka, maisha ya kifahari na hadhi ya juu machoni pa umma.

Waititu alifungwa miaka 12 gerezani na amewasilisha kesi upya kortini akiomba aachiliwe kwa dhamana au pesa taslimu.

Alifungwa kwa kupokea hongo kutoka kwa wanakandarasi alipokuwa Gavana wa Kiambu kati ya 2017-2020.

Jaji Lucy Njuguna alitupilia ombi lake la kwanza la kuachiliwa kwa dhamana mnamo Machi 3 na ataendelea kula maharagwe gerezani akisubiri kesi aliyowasilisha ya kuomba dhamana isikizwe na iamuliwe.

Taifa Leo ilimtembelea Waituti gerezani na mateso na masaibu anayoyapitia yanaweza kulinganishwa na jehanamu au kuzimu ambapo binadamu mwenye dhambi atahangaikia milele kwa mujibu wa vitabu vitakatifu vya dini.

“Gereza si pahala pazuri kwa sababu ni mahali ambapo mawazo mazuri hufa na mtu huathirika kisaikolojia. Hakuna uhuru wowote, hakuna vifaa na sasa najua vizuri sana marafiki zangu,” akasema gavana huyo wa zamani.

“Waona ukiwa na mali, unavutia watu na utafikiria unadhibiti kila kitu. Lakini huwa tunajidanganya kwa kuwa watu huja kukuona kwa sababu wanajua utayatatua matatizo yao,” akaongeza.

Wakati wa mahojiano hayo, Waititu alisimulia kuwa hakuna mtu amekuja kumtembelea tangu asubuhi hiyo huku akisisitiza ataendelea kupambana ili aachiliwe kwa dhamana hata iwe baada ya muda gani.

Mwonekano wa Waititu ni tofauti na yule mwanasiasa Wakenya walimzoea ambaye pia alihudumu kama mbunge wa Kabete, naibu meya wa Nairobi na waziri msaidizi.

Amevalia sare za mahabusu pamoja na champali nyekundu na kusononeka kwake kunajionyesha dhahiri usoni mwake. Hii ni kinyume na kiongozi aliyekuwa akivalia suti na viatu vya bei ghali huku akikitisa mawimbi ya kisiasa na kuwalemea wapinzani.

Gerezani, Waititu kwa hasira anasimulia kuwa amechoshwa na mtindo wa mahabusu kuhesabiwa kila siku.

Kando na kuonekana kupewa makao afadhali kuliko wengine, hakuna jipya huku akilazimika kufyeka na kufanya kazi nyingine za mkono kama mahabusu wengine.

“Hakuna mengi ya kufanya hapa na nimetokea tu kwenye ibada ya kanisa la CIC ambalo liko ndani ya gereza hili. Mahubiri ya leo yalijikita katika kujiinua baada ya kulemwa na mzigo wa maisha,” akasema.

Gereza la Nairobi lina mahabusu karibu 48,000 na inaonekana ‘Baba Yao’ ana mlahaka mzuri na askari gereza huku mmoja aliyejihami akiketi karibu naye wakati wa mahojiano hayo na kufuatilia mambo.

Kiongozi huyo amekiri kuwa maisha yamebadilika kiasi kuwa hata kazi mkono ambazo alikuwa akiwalipa watu wamfanyie sasa inabidi azamie na ni sehemu ya shughuli zake za kila siku.

Kinachomsikitisha na kumkera zaidi kwenye gereza ni kuwa licha ya masaibu yake, hajapata amani.

Wakora wengi wakiwemo wanasiasa wanaoamini alipora mamilioni ya pesa wamekuwa wakija kumshawishi awape pesa eti wana uwezo wa kuwashawishi baadhi ya watu kwenye idara ya mahakama na kutoa uamuzi utakaomtoa gerezani.

“Wiki za kwanza nililetwa hapa zilikuwa mbaya sana kwa sababu kuna watu wanaoamini niliiba mamilioni ya pesa wakati nilikuwa gavana wa Kiambu na sasa nina pesa,

“Wakora na mabroka wamekuwa wakija hapa na kuniambia niwape kati ya Sh10 milioni na Sh15 milioni ndipo watumie ushawishi wao ili niwe huru. Sina pesa hizo na nina hakika siku moja nitatoka hapa nikiwa huru,” akasema Waititu akila matunda kama chakula cha mchana.

Waititu hakupendezwa na mahojiano, alipoulizwa kwa nini alihusisha familia yake na ufisadi uliosababisha afungwe.

“Tatizo lenu wanahabari ni kuwa mnakuja kwa mahojiano na fikira ya kile mngetaka kuandika na kusikiza. Huwa mnaharibu sifa na heshima za watu pamoja na kuvunja familia zao ndiyo maana sitaki kuzungumzia mambo ya familia yangu,” akawaka akiwa amekasirika.

Waititu amekuwa gerezani kwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya kufungwa miaka 12 na kuwekewa faini ya Sh53.7 milioni ili awe huru.