Wakazi walalamika wizi ukichacha karibu na kambi ya kijeshi
WIMBI la uhalifu limekumba maeneo yanayozunguka Kambi ya Jeshi ya Lanet, Kaunti ya Nakuru, huku wakazi wakilalamikia kushambuliwa na kuporwa na majambazi wanaotumia pikipiki hata karibu na vituo vya polisi.
Katika visa vya hivi majuzi, raia kadhaa akiwemo askari wa KDF, akina mama wafanyabiashara na hata viongozi wa Nyumba Kumi wameuawa au kujeruhiwa vibaya.
Hali hii imezua maswali kuhusu usalama wa raia hata karibu na taasisi za kijeshi.
“Kama majambazi wanaweza kumshambulia askari wa jeshi, sisi raia wa kawaida tunalindwa na nani?” alihoji James Kariuki, mkazi wa Lanet.
Katika kisa cha hivi majuzi, William Kamwaro, 49 aliuawa kikatili mnamo Mei 20 alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwa duka.
Mwili wake ulipatikana ukiwa na majeraha ya kudungwa kisu.
“Alikuwa likizoni kwa wiki mbili kutoka Eldoret. Alituacha na huzuni, na hadi sasa polisi hawajatoa taarifa yoyote kuhusu uchunguzi,” alisema mjane wake, Mary Karanja.
Kwa miezi sita iliyopita, takriban watu 10 wameripotiwa kushambuliwa katika eneo hilo. Wengine waliuawa, wakiwemo afisa wa KDF na kiongozi wa Nyumba Kumi.
Msichana mdogo pia aliuawa katika mazingira sawa.
Mashambulizi hayo yamekuwa yakitekelezwa karibu na Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Lanet. Majambazi hutumia mbinu ya kupora kwa ghafla, kisha kutoweka kwa pikipiki.
Wakazi wanalalamikia ukosefu wa magari ya polisi katika vituo vya Lanet, jambo linalochelewesha hatua za maafisa wa usalama kukabili wahalifu.
“Tangu gari letu liharibike mwezi jana, tunafanya doria kwa miguu,” alisema afisa mmoja aliyekataa kutajwa.
Mbunge wa Bahati Irene Njoki pia alikiri kwamba vituo vitatu vya polisi katika eneo lake havina magari wala umeme.
Alisema amewasilisha malalamishi kwa Wizara ya Usalama wa Ndani.
Wakazi sasa wanaitaka serikali kuchukua hatua madhubuti kuimarisha usalama na kuwakamata wahalifu wanaotatiza maisha yao karibu na kambi ya jeshi.