Wakenya walivyochangamkia mwaka mpya licha ya changamoto
FATAKI, vifijo na nderemo, honi za magari na pikipiki, zilitanda angani ilipotimia saa sita kamili usiku wa kuamkia Mwaka Mpya huku mamilioni ya Wakenya wakiaga 2024 na kukaribisha 2025.
Jiji la Nairobi liligeuka kituo cha burudani ambapo tamasha mbili zilifanyika katika eneo la Kencom na katika Jumba la Mikutano la Kimataifa (KICC) na kuwapa fursa maelfu ya Wakenya kusakata ngoma.
Wakenya waliozungumza na Taifa Leo walielezea matumaini kuhusu mwaka mpya huku wakijiandaa kustahimili changamoto zitakazojitokeza.
“Mwaka wa 2024 ulikuwa mgumu na tunashukuru mwaka mpya umeingia. Tulipoteza vijana wengi na tunaomba mwaka huu uwe tofauti,” alisema Bw Mark Muriithi, aliyekuwa miongoni mwa walioshuhudia milipuko ya fataki katika jengo la Old Mutual, Upperhill.
Kwenye barabara kuu ya Nairobi Expressway, mamia ya waendeshaji magari walisimamisha magari yao kutazama maonyesho ya fataki katika majengo kadhaa katikati mwa jiji kuu pamoja na viunga vya Upperhill na Kilimani.
Mamia ya watu walihudhuria misa kuanzia saa moja asubuhi katika makanisa ya Katoliki ya Holy Family Basilica na All Saints Cathedral ambapo saa tatu unusu, waumini waliandika sala za mahitaji yao 2025.
Katika kanisa la Zoe Worship Centre, Kinoo, mamia ya waumini walifika kumshukuru Mungu ambapo kiongozi wao, mchungaji David Nduine, alizungumza kuhusu changamoto zilizogubika 2024 ikiwemo visa tele vya utekaji nyara, ufisadi, mauaji ya wanawake na malumbano baina ya kanisa na serikali.
Wakazi na watalii eneo la Pwani walikaribisha mwaka mpya katika vituo mbalimbali ambapo walitumbuizwa na wasanii akiwemo mwanamuziki wa Tanzania, Zuhura Outhman Soud, almaarufu Zuchu, aliyeongoza burudani ya kuvuka mwaka katika hoteli ya Sarova White sands.Wasanii wa Kenya waliotumbuiza katika tamasha hiyo vilevile ni pamoja na Hart Band, MC Jessy na Mwalimu Rachael.
Huku wapenzi wa burudani wakijivinjari, wanawe marehemu mfanyabiashara tajiri Hasmukh Patel, walikusanyika katika bustani ya Kibarani kugawa vyakula, na mavazi kwa wasiobahatika katika jamii.
Kaka hao walitangaza kuwa watarejelea shughuli za kutoa msaada wa vyakula kwa heshima ya baba yao wakisema mpango huo ulisitishwa na maandamano ya Gen-Z.
Katika Kaunti ya Kilifi, mwanamuziki wa Tanzania, Rajab Abdul Kahali, almaarufu Harmonize au Konde Boy, aliburudisha watu eneo la Water Grounds huku Gavana Abdulswammad Nassir akivukia mwaka Mama Ngina Water Front.
Rais William Ruto alitoa hotuba yake ya mwaka mpya katika ikulu ndogo ya Kisii huku Raila Odinga akiongoza viongozi na wakazi kusherehekea tamasha za Piny Luo Festival 2024, katika Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga.
Rais aliyeandamana na mke wake Rachel kwa maakuli ya mwaka mpya, alivutia umati alipodansi wimbo wa Kasongo wa Kanema ambao umekuwa ukitumika kumdhihaki mitandaoni.
Gavana Fernandes Barasa aliwaongoza mashabiki wa kandanda kushabikia Kombe la Gavana katika uwanja wa Mumias Sports Complex huku idadi kubwa ya wakazi wakifurika makanisani kuvuka mwaka.Katika kaunti ya Nakuru, halaiki ya watu walikusanyika makanisani, barabarani, hotelini na vituo vya umma, kuukaribisha mwaka mpya huku wakazi wakishuhudia mfataki zikilipuka.
Kinyume na hapo awali, fataki zililipuliwa nje na ndani ya kanisa.Katika kanisa la Christ the King Cathedral, Nakuru, waumini wenye bashasha walilipua fataki kukaribisha mwaka mpya baada ya Kasisi Joseph Muchiri kukamilisha mahubiri na kuwahimiza Wakristo kuwa na moyo wa shukrani.
Eneo la Mlima Kenya, wakazi walifurika makanisani, misikitini na vilabu kukaribisha mwaka mpya wakitoa wito kwa serikali kupunguza gharama ya maisha nchini.Fataki zillipuliwa katika kituo cha Nyeri Golf Club, Kaunti ya Nyeri, huku wanaburudani wakisema wanatumai 2025 itakuwa yenye heri.
Viongozi na wakazi Laikipia, Isiolo na Meru Kaskazini walitaka kero la majangili likomeshwe mwaka huu.
Ripoti za Steve Otieno, Ndubi Moturi, Jurgen Nambeka, Winnie Atieno, Philip Muyanga, Mwangi Muiruri, Mwangi Ndirangu, Gitonga Marete, Sammy Kimat George Munene, David Muchui, Francis Mureithi, John Njoroge, Waikwa Maina, Rushdie Oudia, Kassim Adinasi, Ruth Mbula na Shaban Makokha.