Wakenya, wanafunzi waongoza na kushiriki Bungeni katika maonyesho
Kibanda cha Tume ya Huduma ya Bunge (PSC) kilishuhudia msongamano mkubwa wa raia na wanafunzi kutoka zaidi ya shule 152 walioshuhudia na kushiriki katika kikao cha Bunge Mwigo katika Maonyesho ya Kilimo( A.S.K), Mombasa mwaka huu yaliyofungwa rasmi Jumapili Septemba 7 2025.
Shughuli hiyo iligubikwa na furaha, hamasa, udadisi wa dhati na ushiriki wa moja kwa moja wa raia – hali iliyopamba siku ya mwisho ya ushiriki wa Bunge la Kenya katika maonesho hayo ya kitaifa.
Wanafunzi walionekana wakiwa wamevaa mavazi rasmi ya Spika na Karani wa Bunge na Seneti la Kenya, jambo lililoashiria jinsi Bunge limepiga hatua katika juhudi za kufahamisha umma shughuli zake na kuvunja dhana hasi kuhusu shughuli zake..
Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo ya Bunge la Kitaifa, John Mutunga, alisifia mpango huo akisema ni hatua kubwa katika kukuza uelewa wa wananchi – hasa vijana – kuhusu majukumu ya Bunge.
“Tunataka vijana wetu wajifunze mapema kuhusu nafasi ya Bunge katika uongozi. Ili wawe viongozi wa kesho, ni muhimu kuwapa fursa ya kupata uzoefu wa moja kwa moja wa jinsi Bunge hufanya kazi,” alisema Bw Mutunga.
Wanafunzi walipata nafasi ya kuzungumza na maafisa wa Bunge waliowafundisha hatua kwa hatua kuhusu mchakato wa kikao cha Bunge, kuanzia kufungua kikao hadi kuwasilisha hoja na kupiga kura.
Kilele cha shughuli katika kibanda hicho kilikuwa mjadala na kipindi cha maswali ambapo wanafunzi wanne walishiriki pamoja na watumishi wa Bunge, na washindi wakatunukiwa medali kama njia ya kutambua juhudi zao na kuweka kumbukumbu ya pekee.
Wanafunzi waliongoza pia kikao cha Bunge Mwigo kilichojadili masuala ya Kilimo, chini ya uenyekiti wa Bw Mutunga. Shule zilizoshiriki ni pamoja na Shule ya Msingi ya Nyali, Shule ya Msingi ya Ganjoni,Shule ya Upili ya Khamisi, na Shule ya Mtongwe.
Walimu waliowasindikiza wanafunzi walipongeza PSC kwa kubuni njia ya kufundisha kupitia vitendo. Walibainisha kuwa elimu ya vitendo huwasaidia wanafunzi kuelewa kwa urahisi zaidi.
“Tumejifunza mengi. Mbinu hii ya Bunge kufika mashinani imewafikia hata wale ambao hawawezi kufika Nairobi. Kuonyesha taratibu kwa njia rahisi kumewasaidia wanafunzi kuelewa vizuri zaidi,” alisema Mwalimu kutoka Shule ya Msingi ya Nyali.
Tume ya Huduma ya Bunge inaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kuwawezesha vijana kupitia programu za kuwafikia mashuleni, kwa lengo la kuweka msingi wa kuandaa viongozi bora wa siku zijazo.
Mpango huo pia unalenga kukuza uzalendo, mshikamano wa kitaifa, amani na ushirikishaji wa vijana katika maamuzi ya umma.
Kamati ya Mawasiliano ya Umma ya Tume hiyo ilisisitiza kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Kenya ya 2010, ni muhimu kwa wananchi kushirikishwa katika kila hatua ya mchakato wa bajeti.
Ushirikishaji huu unawezekana tu iwapo wananchi wanaelimishwa vya kutosha kuhusu vipaumbele, vyanzo vya fedha na matumizi ya rasilimali.
Wabunge waliokuwepo waliongeza kuwa wanatambua historia ndefu ya utawala wa Bunge kwa kutumia vielelezo vinavyobeba alama na historia tajiri ya taasisi hiyo muhimu nchini