Wakili wa Gen-Z ageuka mwiba kwa utawala wa Ruto
WAKILI ambaye alijizolea umaarufu sana kwa kuwawakilisha Gen-Z wakati wa maandamano sasa amegeuka mwiba kwa utawala wa Rais William Ruto baada ya kuanika miradi iliyoanzishwa zamani, ikakwama na inaendelea kuzinduliwa, raia wakipoteza mabilioni ya hela.
Wakili Morara Kebaso alipata umaarufu mkubwa akishiriki maandamano ya Gen-Z na wakati huo huo pia alikuwa akiwawakilisha vijana ambao walinyakwa na kuzuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.
Baada ya maandamano hayo kuisha nguvu, Bw Kebaso ameibuka na mbinu nyingi ambapo anasafiri maeneo mbalimbali na kufichua miradi ambayo imezinduliwa zaidi ya mara mbili na Rais Ruto.
Aidha, ameanika pia miradi mbalimbali ya serikali ambayo imekwama ilhali tayari serikali imetumia mabilioni ya pesa kuizindua.
Mbali na kuwa na ufuasi mkubwa mtandaoni, wengi wa Gen-Z sasa wanamwona kama sauti yao kushinikiza serikali iwawajibikie raia.
Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, Bw Kebaso alifichua kwa nini alishiriki maandamano hayo; kwa sababu alihisi kuwa vijana walikuwa wanapigania haki na uwajibikaji kutoka kwa serikali.
“Maandamano hayo yalipoanza, mimi na mke wangu tulijiunga na Gen-Z katika barabara za Nairobi. Hakuna maandamano ambayo nilikosa kwa sababu tulikuwa tunasaka uwajibikaji na pia kupambana na ufisadi kwenye utawala wa sasa.
“Vita vyetu vilikuwa vya kupigania Kenya bora na hatujatimiza hilo,” akasema Bw Kebaso.
Kwenye mojawapo ya ufichuzi wake, Bw Kebaso alikabana koo na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed kuhusu kuzinduliwa kwa barabara ambazo zilikuwa zimeshaanzishwa na utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta eneo la Gusii.
Rais Ruto alikuwa kwenye ziara ya kuzindua miradi mbalimbali ya serikali katika eneo hilo.
Wakili Kebaso alitaja barabara za Metembe-Marani-Kegogi-Nyaore ambazo ziko katika eneobunge la Kitutu Chache Kusini na Kitutu Chache Kaskazini, Kisii akisema ujenzi wazo ulizinduliwa enzi za Bw Kenyatta mnamo 2016.
“Viongozi kutoka jamii za Abagusii walikuwa wanamsifu Rais Ruto kana kwamba ni Mungu. Ujenzi wa barabara hiyo ulizinduliwa na Bw Uhuru 2016 kisha Rais Ruto akauzindua tena alipokuwa Kisii. Ni maendeleo gani Rais alileta Kisii?” Bw Kebaso akauliza kwenye ukurasa wa X.
Bw Mohamed alimjibu na kutoa ufafanuzi kuwa mradi huo ulikwama kutokana na kuzembea kwa mwanakandarasi wa awali na mwingine akapewa tenda mnamo Machi.
Msemaji wa Ikulu aliongeza kuwa ujenzi huo ulirejelewa mnamo Juni ndiposa Rais alienda kuuzindua tena.
“Wakati mwanakandarasi wa awali akiondolewa alikuwa amekamilisha kilomita 27 kwa miezi 77 ilhali alikuwa na miezi 30 ya kufanya kazi hiyo. Rais Ruto alizindua mradi huo tena kama njia ya kutimiza ahadi yake ya kukamilisha miradi yote iliyokwama,” akasema Bw Mohamed.
Licha ya ufafanuzi huo, Wakenya wengi kwenye X walimuunga mkono wakili huyo huku wengine wakitembelea barabara hizo kukanusha madai ya serikali.
Katika ziara zake, wakili huyo maarufu amekuwa akifuatilia na kukagua miradi iliyofadhiliwa na serikali katika kaunti za Nyandarua, Kiambu, Uasin Gishu, Kajiado, Murang’a, Nandi, Kakamega, Vihiga na Kisumu.
Amebaini kuwa miradi mingi iliyoanzishwa imekwama au haijaanza kabisa kwenye ziara zake katika kaunti hizo.
Bw Kebaso ambaye anamiliki kiwanda cha kutengeneza bidhaa, anasema kuwa amepata msukumo wa kuwaambia Wakenya ukweli kuhusu jinsi ambavyo ufisadi umenoga serikalini.
“Lengo langu ni kuanika miradi iliyokwama na ile ambayo haijaanzishwa licha ya ahadi nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa na utawala wa Rais Ruto,” akasema.
“Gen Z walipokuwa na maandamano, ilikuwa lazima nijiunge nao kupigania Kenya bora,” akasema Bw Kebaso. Baba huyo wa watoto wawili; mvulana na msichana, anasema kuwa matakwa ya Gen Z bado hayajaafikiwa.
Kuhusiana na vitisho dhidi ya maisha yake, Bw Kebaso amesema hatetereki.
“Sote kwa kipindi kimoja cha uhai wetu tutakufa. Nimepokea vitisho kutoka kwa watu ambao naamini wametumwa na serikali lakini sijali,” akasema.
Wakenya wengi hugharimia ziara zake hizo lakini anasema wanaotoa pesa au kumchangia hufanya hivyo kwa hiari.
Bw Kebaso anafuata nyayo za babu yake marehemu George Morara ambaye alikufa kupitia ajali ya barabarani iliyozua maswali mnamo 1970.
Akiwa na umri wa miaka 34 pekee na pia mbunge wa West Mugirango, Bw George kabla ya mauti yake alikuwa mwiba wa utawala wa Mzee Jomo Kenyatta, hasa kwa kuibua maswali mengi kuhusu mauaji ya Tom Mboya mnamo 1969.