Walevi wa ‘tot’ walia hawawezi kumudu bei ya ‘mzinga’
NA MWANGI MUIRURI
SERIKALI imetoa ilani kwamba pombe ya makali itakayokuwa zikipatikana sokoni huenda ziwe zikipakiwa katika chupa kwa vipimo vya milimita 750 almaarufu mzinga.
Hii ina maana kwamba mlevi anayehitajika sasa katika soko ni yule atakayekuwa na uwezo wa kujinunulia mzinga mzima, serikali ikitishia kwamba “hata huenda kipimo hicho kikadiriwe upya ili kiwe zaidi ya milimita 750”.
Awali, vipimo sokoni vilikuwa vya milimita 250 na 500 lakini wauzaji wakiwa wabunifu na kuiuza kwa vipimo aina ya ‘tot’ na pia kugawa zile za bei za chini kwa vipimo hata vya Sh10.
“Mimi kwa maoni yangu nafikiria wanaopendekeza hizi sheria licha ya kutoelewa soko la pombe, hata wao hawajielewi kabisa. Mzinga ule wa bei ya chini kwa sasa katika baa ni Sh700,” akasema Bw Stephen Mwangi, mkazi wa Murang’a
Alisema vibarua vya chini mashinani kwa siku ni Sh300.
“Eti nifanye kazi kwa siku tatu ndipo niweze kuingia kwa baa? Wasitusukume kunywa pombe ya haramu,” akasema.
Alisema kwamba pombe ikianza kupakiwa kwa vipimo hivyo, viwanda vitafungwa, baa nyingi zisambaratike na wengi wa wateja wahangaike hadi kuanza kusaka ulevi katika madang’uro haramu na hivyo basi kuua nafasi za ajira na kuhatarisha maisha ya walevi.
Katika mapendekezo mapya ambayo yametolewa yakinuia kuzima ulevi kiholela, baa zote zilizo karibu na maeneo ya makazi, shule na eneo la ibada zitafungwa huku magari ya kusafirisha pombe na sigara zikihitajika kuwa na rangi moja spesheli na uchukuzi uwe tu ni kati ya saa 12 asubuhi na saa 12 jioni.
Wenye majengo ya kukodisha katika mitaa ya makazi na vijijini watasakamwa wenyewe ikiwa watakodisha manyumba kwa wauzaji vileo.
Vilevile, maafisa wote wanaofanya kazi katika vitengo vya kiusalama watalazimika kufunga biashara zao za baa kwa walio nazo la sivyo wajiuzulu ili wakimbizane na biashara ya kuuza ulevi.
Sheria hizo zinaonya kwamba hakuna aliye na ruhusa ya kuuza shisha nchini au hata kupatikana ukiipigia debe kupitia matangazo.
Mikakati hiyo inavumishwa chini ya ushirikishi wa naibu wa rais Bw Rigathi Gachagua ambaye anateta kwamba viwango vya ulevi nchini ni vya kusikitisha kiasi kwamba hata nguvu za kiume kwa wengi vimepotea hivyo basi kunyima taifa vizazi vya kesho.
Huku wengi wakitoa tahadhari kwamba vita vya ulevi huwa vigumu na vinaweza vikazima nyota za kisiasa, Bw Gachagua ameshikilia kwamba “ikiwa mimi binafsi nitapoteza umaarufu wa kisiasa kutokana na vita dhidi ya ulevi, basi na iwe hivyo, sijali”.
Aliongeza kwamba “hao walio katika biashara hiyo ya kuuza ulevi wa kuua wengine hukesha wakijigamba kwamba wataangusha wanasiasa na wazime ari zao za kuchaguliwa”.
Akiwajibu, Bw Gachagua aliwasuta kama “wasio na wingi, uwezo na umaarufu wa kushawishi matokeo ya kisiasa”.