Habari za Kitaifa

Walimu wakuu: Julius Migos ni Waziri muongo

Na WINNIE ATIENO March 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WALIMU wakuu nchini wamekanusha ripoti kutoka Wizara ya Elimu kwamba serikali ilituma mgao wote wa fedha za elimu (capitation) za muhula wa kwanza wiki iliyopita.

Aidha, walimu hao chini ya muungano wa walimu wakuu nchini (KESSHA) walisema bado wanadai serikali fedha za muhula wa kwanza.

Walisema wanadai malimbikizi ya madeni ya Sh7 bilioni kwa muhula wa kwanza wa mwaka huu huku ikisalia wiki mbili kabla shule zifungwe kwa muhula wa pili.

Shule zote zinatarajiwa kufungwa ifikapo Aprili 4, 2025 kwa mujibu wa kalenda ya elimu ya mwaka huu iliyochapishwa Januari mwaka huu.

“Tunaitaka serikali, kuipa kipa umbele sekta ya elimu hasa ufadhili wa masomo ambapo kuna changamoto kubwa ikiwemo kucheleweshwa kwa fedha inayoathiri masomo ya wanafunzi wetu,” alisema mwenyekiti wa muungano wa walimu wakuu nchini Bw Willy Kuria.

Bw Kuria ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wavulana ya Muranga pia alishutumu hatua ya wizara hiyo ya kuwaamrisha kupeana vyeti vya wanafunzi waliomaliza shule za sekondari licha ya deni la karo ya shule.

“Deni hilo la karo ya shule hutozwa kutokana na masomo wanafunzi hupokea shuleni. Itakuwaje leo tunaambiwa tuwapatie vyeti hivyo bila ya kujukumika kulipia deni letu? Huu sio uamuzi bora sababu serikali inafahamu madeni tuliyonayo,” aliongeza Bw Kuria.

Bw Kuria ambaye anazungumza kwa niaba ya walimu wakuu 10,000 kote nchini alisema ipo haja ya wanafunzi kulipa madeni yao kabla ya kuchukua vyeti hivyo vya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE).

Machi 17, 2025, Waziri wa Elimu Bw Julius Migos aliagiza shule zote nchini kupeana vyeti vya KCSE kwa wanafunzi wenye madeni.

Vile vile, Bw Migos alitangaza kuwa serikali imetuma mgao wa fedha za elimu wa Sh14 bilioni kwa shule za sekondari kwa muhula wa kwanza.

Hata hivyo, walimu wakuu walipinga ripoti hiyo wakisema fedha zilizotumwa ni nusu ya zile zinazotakiwa kupeanwa.

“Tunadai serikali Sh2, 303 kwa kila mwanafunzi kwa muhula huu, kwa jumla tunadai serikali takriban Sh7 billioni kwa muhula wa kwanza wa mwaka huu,” aliongeza mwalimu huyo mkuu.

Alisema wanakabiliwa na changamoto ya kulipa mishahara kwa wafanyikazi wao hasa walimu wanaoajiriwa na bodi za shule hizo.

Serikali hugharamika kulipa Sh22, 244, kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.

“Muhula wa kwanza serikali inafaa kulipa asilimia 50 ambayo ni Sh11, 122 lakini tumepokea Sh8, 819,” alisema.

Muhula wa pili serikali inafaa kulipa Sh6, 673 ikiwa asilimia 30 ya karo huku muhula wa tatu ikisalia asilimia 20 ikiwa ni Sh4, 448.