Waluke, Wakhungu walivyofaulu kuthibitishia korti kwamba hawakula Sh313 milioni za NCPB
MAHAKAMA ya Rufaa ilifutilia mbali vifungo vya miaka 67 jela dhidi ya Mbunge wa Sirisia, Bw John Walukhe na aliyekuwa mshirika wake wa kibiashara Grace Wakhungu ambao walikuwa wameshtakiwa kwa kujipatia Sh313 milioni kwa njia ya ulaghai kutoka kwa shirika la serikali.
Wawili hao walikuwa wamefungwa kwa zaidi ya miaka 60 kila mmoja, au kulipa faini ya zaidi ya Sh1 bilioni baada ya kupatikana na hatia ya kupokea kwa njia ya ulaghai pesa kutoka kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kwa mahindi, ambayo hawakuwasilisha.
“Mwishowe, tumeridhika kwamba waliokata rufaa wamethibitisha kesi ya kuturuhusu kukubali rufaa. Rufaa hiyo inakubaliwa ipasavyo, na hukumu zilizotolewa zimefutwa,” Majaji Asike Makhandia na Patrick Kiage walisema.
Jaji Abida-Ali Aroni alikataa kutia saini uamuzi huo. Bw Walukhe na Bi Wakhungu walisema malipo hayo yalitokana na upatanishi na sio uuzaji.
Kupitia wakili Paul Muite, Bi Wakhungu alisema walichopata ni sehemu ya pesa walizopaswa kulipwa.
“Hakuna kesi ya ulaghai inayoweza kutokana na agizo la mahakama ambalo halikusimamishwa au kubatilishwa. Kama walalamishi wangekuwa wameenda River Road na kutengeneza agizo feki, ingekuwa tofauti,” alisema.
Wawili hao na kampuni yao, Erad Supplies & General Contractors, walipokea zaidi ya Sh313 milioni kutoka NCPB kwa uuzaji uliodaiwa kuwa feki wa tani 40,000 za mahindi kwa serikali mwaka wa 2004.
Bw Muite alisema baada ya kukosa kutupilia mbali uamuzi huo, NCPB ilianza kesi katika EACC.
Alisema Erad Supplies ilipeleka kesi hiyo kwa upatanishi ikitaka fidia ya jumla na maalum kwa ukiukaji wa mkataba.