Wanafunzi 13 wajeruhiwa katika mkasa wa moto Machakos
POLISI wamethibitisha kuwa wanafunzi 13 walijeruhiwa kufuatia mkasa wa moto ulioteketeza mabweni mawili katika Shule ya Upili ya Katoloni iliyoko Kaunti ya Machakos.
Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Machakos Patrick Lobolia, Jumapili, Septemba 15, 2024 aliambia Taifa Dijitali kwamba majeruha hayo yalitokana na mkanyagano wa wanafunzi waliokuwa wakitoroka baada ya moto kutokea mwendo wa saa tatu za usiku, Jumamosi, Septemba 14.
“Wanafunzi hao 13 walikimbizwa katika Hospitali ya Machakos Level 5 ambako walitibiwa na kuruhusiwa kurejea shuleni. Walipata majeraha madogo wakitoroka,” Lobolia akaeleza, kwa njia ya simu.
Afisa huyo alisema wanafunzi wote walikuwa madarasani wakisoma usiku moto ulipotokea.
“Hakuna mwanafunzi aliyekuwa ndani ya bweni; wote walikuwa madarasani. Lakini waliingiwa na woga baada ya kamsa kupigwa kwamba shule ilikuwa ikiteketea na ndipo wakaanza kutorokea usalama,” Bw Lobolia akasema.
Moto huo, ambao chanzo chake hakijabainishwa, ulidhibitiwa mwendo wa saa nne na nusu za usiku.
“Moto huo uliteketeza nguo, vitabu, masanduku na malazi ya wanafunzi hao kabla ya kudhibitiwa. Maafisa wetu wameanza uchunguzi kubaini chanzo chake,” Bw Lobolia akasema.
Kamanda huyo wa polisi alisema wanafunzi wote waliokuwa shuleni humo usiku huo wako salama.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga