Wanafunzi kurejea shuleni muhula wa mitihani bila pesa
Maelfu ya wanafunzi kote nchini wanarejea shuleni kesho kwa muhula wa tatu ambao ni mfupi zaidi na wa mitihani mingi zaidi katika kalenda ya masomo. Muhula huu utadumu kwa wiki tisa pekee, lakini umejaa mitihani ya kitaifa na tathmini muhimu.
Katika kipindi hiki, watahiniwa watafanya mitihani mbalimbali kama vile Kenya Primary School Education Assessment (KPSEA) kwa wanafunzi wa Gredi 6, Kenya Junior School Education Assessment (KJSEA) kwa wanafunzi wa Gredi 9, na Kenya Certificate of Secondary Education (KCSE) kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne, itakayofanyika kuanzia Oktoba hadi Novemba.
KPSEA hupima utayari wa kujiunga na Sekondari Msingi, KJSEA, kwa mara ya kwanza, itawahusisha wanafunzi wa Gredi 9 wanaotarajiwa kuingia Sekondari Pevu chini ya mfumo wa Umilisi na Utendaji (CBC). Takribani wanafunzi milioni 1.2 wanatarajiwa kufanya mtihani huu.
Kuchagua wanafunzi kujiunga na Sekondari Pevu kutafanyika kwa misingi ya mkondo waliouchagua, masomo wanayopendelea, na matokeo ya jumla ya tathmini ya Gredi 6 hadi 9.
Mikondo katika Sekondari Pevu ni mitatu: Sayansi Jamii, Sanaa na Michezo, na Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM). Hata hivyo, Hisabati, Kiingereza, Kiswahili, na Huduma kwa Jamii ni lazima kwa wanafunzi wote.
Kwa KCSE, huu ni mtihani wa mwisho wa kitaifa kwa sekondari, na unahusisha maandalizi makubwa. Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari (Kessha), Bw Willy Kuria, alisema muhula huu ni muhimu sana na unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walimu, na serikali.
“Iwapo mzazi anataka mwanawe afaulu, ni muhimu kutambua kuwa shule hazijapokea mgao kamili wa fedha za serikali. Ikiwa bodi za shule zitawaomba wazazi kusaidia kununua vifaa vya mitihani, basi wazazi wasisite kusaidia,” alisema Bw Kuria.
Kuria, ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Murang’a, alielezea hofu kuhusu gharama kubwa ya kuendesha muhula wa tatu hasa kwa shule za kutwa ambazo zinakabiliwa na ukosefu wa fedha kwa ajili ya vifaa vya mitihani ya vitendo kama sayansi, kilimo na lugha za kigeni.
Kulingana na Kessha, shule hazijapokea mgao wa muhula wa tatu. Kwa muhula wa pili, walitarajia Sh6,673 kwa kila mwanafunzi lakini walipokea Sh3,471 tu upungufu wa Sh3,202 kwa kila mmoja. Muhula wa kwanza walitarajiwa kupata Sh11,122 lakini walipokea Sh8,818 pekee.
Kwa jumla, serikali inadaiwa zaidi ya Sh18 bilioni kwa muhula wa kwanza na wa pili. Kulingana na mpango wa mwaka, shule zinapaswa kupokea asilimia 20 ya Sh22,000 kwa mwanafunzi kwa muhula wa tatu.
Waziri wa Elimu, Bw Julius Ogamba, alikiri kuwa fedha bado hazijatolewa lakini alisema wizara yake inashughulikia suala hilo haraka.
Katika kikao cha bunge mwezi Juni, Ogamba alifichua kuwa shule za msingi na sekondari za umma zina madeni yanayokaribia Sh64 bilioni, kutokana na ucheleweshaji wa mgao wa fedha miaka ya nyuma.
Mwenyekiti wa Muungano wa Wazazi Kitaifa, Bw Silas Obuhatsa, aliwataka wazazi kuwaandaa kisaikolojia watoto wa Gredi 6, Gredi 9, na Kidato cha Nne kwa mitihani yao ya mwisho, na kuhakikisha wanalipa karo kwa wakati.
“Wazazi watoe usaidizi wa kiakili na kifedha kwa watoto. Lakini walimu wakuu wasiwafukuze wanafunzi kwa sababu wengine hawajalipwa mishahara ya Agosti,” alisema.
Viongozi wa walimu kutoka Kuppet na Knut walihimiza maandalizi mazuri kwa wanafunzi huku Baraza la Mitihani la Kenya (Knec) likieleza kuwa mipango yote iko tayari. Mkurugenzi Mtendaji wa Knec, Dkt David Njengere, alisema ratiba ya KCSE tayari imetolewa ili kuruhusu maandalizi mapema.