Habari za Kitaifa

Wanajeshi kulipia mlo kambini ruzuku ya chakula ikiondolewa

Na MOSES NYAMORI, ROSELYNE OBALA January 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) wameamuru kuondolewa kwa mpango wa ruzuku ya chakula kwa wanajeshi kuanzia Julai 1, 2025, kulingana na stakabadhi zilizoonwa na Taifa Leo.

Katika mpango huo mpya, KDF inataka kuacha mpango wa sasa wa chakula cha mchana unaofadhiliwa na Hazina ya Kitaifa hadi mfumo wa kulipia chakula ambacho mwanajeshi anakula na ambao umezua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wanajeshi.

Katika agizo la Januari 17, 2025 lililotiwa saini na Meja Jenerali MN Hassan, KDF inasema uamuzi huo umesababishwa na utepetevu na utendakazi wa mfumo wa sasa.

Afisa mkuu wa jeshi aliyezungumza na Taifa Leo bila kutaja jina kutokana na uzito wa suala hilo alisema utekelezaji wa mfumo huo mpya unatarajiwa kuokoa kati ya Sh2 bilioni na Sh3 bilioni za mlipa ushuru kila mwaka. Afisa huyo alisema mpango wa sasa wa ruzuku una uvujaji ambao unaendelea kuwagharimu walipa kodi.

Lakini mpango huo umepokelewa kwa hisia tofauti katika kambi za jeshi, huku baadhi ya wanajeshi, ambao walizungumza na Taifa Leo kwa sharti la kutotaja majina yao, wakihisi kuwa mfumo unaopendekezwa unaweza kuwaletea hasara.

Baadhi walisema wako na mikopo, jambo ambalo walisema huenda likawalazimu kukosa chakula iwapo mfumo huo utatekelezwa.

Si mara ya kwanza KDF kujaribu kutekeleza mfumo huo mpya.

Majaribio ya awali, ikiwa ni pamoja na wakati wa uongozi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Robert Kibochi hayakufaulu. KDF tangu wakati huo imekuwa ikiweka miongozo inayolenga kuhakikisha utekelezaji mzuri wa mfumo huo bila tatizo.

Miongozo hiyo ilijumuisha kuanzishwa kwa “mpango wa kina wa uhamasishaji kwa wanajeshi wote ili waweze kuuelewa mfumo huo unaohusu kulipia chakula wanachokula”.

Katika jibu rasmi kwa maswali ya Taifa Leo, Wizara ya Ulinzi ilisema uamuzi huo umesababishwa na haja ya kurekebisha mgao wa bajeti, ufanisi katika matumizi ya rasilimali za serikali pamoja na kuwezesha upatikanaji wa aina mbalimbali za mlo kukidhi matakwa ya mtu binafsi.

Wizara pia ilisema kuwa hatua hiyo inalingana na mazoea bora ya kijeshi kikanda na kimataifa.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA