Wanaohitimu Aga Khan wahimizwa kutetea uvumbuzi
WAHIITMU wa Chuo Kikuu cha Aga Khan wamehimizwa kukumbatia uvumbuzi, ushirikishaji na huduma kwa wanadamu wote.
Akiongoza mahafali katika chuo kikuu hicho jijini Nairobi, Binti mfalme Zahra Aga Khan, alisisitiza kuwa dhamira ya taasisi hiyo ni kuwapa wanafunzi ujuzi wa kukabiliana na changamoto za ulimwengu halisi na kuinua jamii.
“Baba yangu daima aliona chuo kikuu hiki kama taasisi ya kimataifa ya aina yake – ambayo hutumikia jamii zinazoendelea, kukumbatia tofauti za kitamaduni, na kukuza uvumbuzi. Lakini maono haya yana maana gani kwetu leo? Inamaanisha athari za kimataifa, maendeleo, na ushirikishaji katika kila nyanja,” Binti Mfalme Zahra alisema.
Wakati wa hafla hiyo katika Chuo Kikuu cha Aga Khan jijini Nairobi, Mwanamfalme Zahra alisisitiza jukumu la elimu katika kuleta mabadiliko katika jamii, akiwataka wahitimu kutumia ujuzi wao kubadilisha maisha.Alisisitiza kuwa nguvu ya chuo kikuu haiko katika miaka lakini katika kuathiri vizazi na kuunda viongozi wa baadaye.
“Nguvu ya taasisi hii haipimwi kwa miaka lakini katika kuathiri vizazi,” alibainisha, akisisitiza jukumu la muda mrefu la chuo kikuu katika kuunda viongozi. “Ikiwa ningetoa ushauri mmoja, itakuwa hivi: Jitahidi kila wakati kuwa bora kuliko ulivyokuwa jana.”
Binti Mfalme Zahra alikubali changamoto zilizo mbele yao ila aliwakumbusha wahitimu kwamba uvumilivu utaleta ufanisi wa maana.
“Safari ya mbeleni haitakuwa rahisi kila wakati, lakini inafaa. Taasisi hii imekuza viongozi, wavumbuzi na wa kuleta mabadiliko. Itaendelea kufanya hivyo kwa vizazi vijavyo,”alisema.
Akithibitisha tena imani ya taasisi hiyo katika werevu na uwezo wa kibinadamu kubadilika, Binti Mfalme Zahra aliangazia dhamira yake ya kuunda mifumo inayowezesha watu binafsi na jamii.
“Baba yangu aliamini katika ubinadamu – wazo kwamba furaha na ustawi vinapaswa kuwa kiini cha juhudi zetu za kuboresha mustakabali wa sayari yetu. Alikuwa na imani katika nguvu ya elimu na uvumbuzi,” alisema.