Habari za Kitaifa

Wapelelezi wa kampuni iliyodaiwa kupunja raia Sh720 milioni wahamishiwa mbali

Na SIMON CIURI October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAAFISA wa upelelezi kutoka Nairobi waliochunguza kampuni ya ajira ng’ambo ambayo ilipokonywa leseni na serikali baada ya madai kwamba iliwalaghai wanaotafuta kazi Sh720 milioni wamehamishwa hadi vituo vya mbali.

Afisa Mkuu wa Upelelezi wa Jinai eneo la Nairobi Njeru Nthigah ambaye alikuwa akiongoza uchunguzi dhidi ya Vintmark Travel Agency Ltd inayomilikiwa na Bw Ceaser Kingori ni miongoni mwa maafisa 12 wa polisi waliohamishwa hadi vituo nje ya Nairobi, baadhi vikiwa karibu na Msitu wa Boni, Kilifi, Samburu na Garissa.

Bw Nthigah alikuwa ameunda timu ya wapelelezi sita kuchunguza kampuni ya Vintmark Travel Agency Ltd kuhusu madai kuwa iliwalaghai watu kwa kuwaahidi kazi hewa nchini Canada, Uingereza, Dubai, miongoni mwa nchi nyingine za Ulaya na Uarabuni.

Wakati huo, Bw Nthigah aliambia Taifa Leo kwamba Bw Kingori alipuuza wito wa kurekodi taarifa baada ya malalamishi mengi kuwasilishwa dhidi ya kampuni yake.

Badala yake alichapisha picha yake akiwa na Waziri Alfred Mutua katika ziara ya Rais William Ruto nchini Ujerumani.

”Imefikia hatua sasa Bw Kingori amekuwa mgumu na alipoitwa wiki jana na mmoja wa maafisa wa uchunguzi kurekodi taarifa zaidi baada ya kundi jingine kuibuka likidai kuwa kampuni ya Vintmark Tours Travel Ltd imewalaghai, alijibu kwamba alikuwa Ujerumani na akasambaza picha yake na waziri. Ninapanga kuwa na mkutano na Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii, Alfred Mutua na kumweleza jinsi ulaghai ulivyo mkubwa katika mashirika ya kuajiri na hatua ambazo zinafaa kutekelezwa kwa kasi kwa sababu hali hiyo inatia wasiwasi,” Bw Nthigah aliambia Taifa Leo wakati huo.

Waziri Mutua kisha aliambia Taifa Leo kwamba maajenti wengi waliokuwa sehemu ya ujumbe wa Ujerumani walikuwa wamelipa tikiti zao wenyewe baada ya kuomba idhini ya serikali.

Jumanne, Taifa Leo ilithibitisha kuwa Bw Nthigah alihamishwa siku moja baada ya ufichuzi kuhusu Bw Kingori. Nafasi yake ilichukuliwa na Bw Benson Kasyoki ambaye alikuwa Afisa Mkuu wa Upelelezi wa Jinai eneo la Mashariki.

Bw Nthigah ametumwa eneo la Magharibi kama Afisa wa Upelelezi wa Jinai. Wengine katika timu aliyokuwa ameunda wamehamishwa hadi Kilifi, Samburu na Garissa.

Taifa Leo iliwasiliana na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kuhusu uhamisho huo na kama ulikuwa adhabu kwa uchunguzi dhidi ya Vintmark Travel Agency Ltd kama ilivyodaiwa.

Bw Kanja alisema hakuwa na ufahamu kuhusu matukio hayo lakini akaongeza kuwa itakuwa jambo la kutia wasiwasi ikiwa ndivyo ilivyokuwa.

Bw Kanja badala yake alielekeza Taifa Leo kwa mkuu wa DCI Mohammed Amin.

”Sifahamu habari hizo na niruhusu nikuelekeze kwa Bw Amin. Lakini hilo lingeshtua ikiwa kweli ndivyo ilivyotokea. Labda yeye (Amin) hata hafahamu,’’ Bw Kanja aliambia Taifa Leo.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA