Habari za Kitaifa

Washauri haramu? Uteuzi wa Ndii, Kuria, Mutua wapingwa kortini

Na SAM KIPLAGAT May 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKILI wa Nairobi, Bw Suyianka Lempaa, amewasilisha kesi mahakamani akiomba amri ya kuwashurutisha washauri wa Rais William Ruto warejeshe mamilioni ya pesa walizolipwa kama mishahara na marupurupu, akisema uteuzi wao ulifanywa kinyume cha sheria.

Katika kesi iliyowasilishwa kwa dharura, Bw Lempaa anasema kuwa kuanzishwa kwa nyadhifa na kuajiriwa kwa maafisa hao kama washauri wa rais na afisi wanazoshikilia kulifanyika kinyume cha katiba na sheria za nchi.

Wakili huyo ametaja washauri 14 wakiwemo Prof Makau Mutua (Masuala ya Kikatiba), Moses Kuria (Mshauri Mkuu wa Uchumi), David Ndii (Mwenyekiti – Baraza la Washauri wa Kiuchumi), Prof Edward Kisiangani (Mshauri Mkuu), Dkt Monica Juma (Mshauri wa Usalama wa Kitaifa) na Joseph Boinnet (Naibu Mshauri wa Usalama wa Kitaifa).

Pia, ametaja Bw Jaoko Oburu (Uwezeshaji wa Kiuchumi na Maisha Endelevu), Dkt Nancy Laibuni (Mwanachama – Baraza la Washauri wa Kiuchumi), Harriette Chiggai (Mshauri wa Haki za Wanawake) na Prof Abdi Guliye (Mshauri wa Usimamizi wa Mifugo na Malisho).

Bw Lempaa amesema kuwa baadhi ya kazi zinazotekelezwa na washauri hao zinaweza kufanywa na watumishi wa umma katika idara mbalimbali za serikali.

“Kujaa kwa washauri ndani ya Utumishi wa Umma kunakiuka matumizi bora ya fedha za umma na kutokuwa na sheria au kanuni kuhusu idadi ya washauri wanaoweza kuteuliwa na rais si ruhusa ya kujaza utumishi wa umma na watu wanaoteuliwa kisiasa,” alisema kwenye ombi lake.

Wakili huyo anataka mahakama iagize washauri hao kurejesha kwa hazina ya serikali fedha zote na marupurupu waliolipwa.

Pia, anataka Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) kufanya ukaguzi ndani ya siku 60 baada ya uamuzi wa mahakama, ili kubaini afisi zote zilizoanzishwa na Rais na serikali kuu kinyume na katiba na sheria.

“Rais na maafisa wa serikali kuu wameunda afisi nyingi na kuzijaza watu kinyume cha katiba,” aliongeza.

Wakili huyo anahoji kuwa, afisi hizo hazikuanzishwa kwa mujibu wa mapendekezo ya PSC.

Huku kesi hiyo ikisubiri kusikilizwa na kuamuliwa, Bw Lempaa anataka mahakama itoe amri Rais asitishe uteuzi zaidi wa washauri.

Anasema aliamua kwenda mahakamani kwa sababu hakuna sheria au kanuni zinazobainisha idadi ya washauri ambao rais anaweza kuwateua, jambo linalotoa mwanya kwa rais kuajiri watumishi wa umma kinyume na maadili na kanuni za utumishi wa umma.

Aidha, anasema ukosefu wa sheria au kanuni kuhusu idadi ya washauri wanaoweza kuteuliwa na rais si ruhusa ya kujaza utumishi wa umma na wateule wa kisiasa.

“Tangu serikali ya Kenya Kwanza iingie madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, rais ametengeneza utumishi wa umma sambamba na utumishi wa umma wa kawaida,” alisema.

Aliongeza kuwa hakukuwa na ushindani kubaini, miongoni mwa masuala mengine, uwezo wa walioteuliwa kwenye afisi hizo.

“Vilevile, kwa sababu mchakato wa kuanzisha na kuteua washauri ulikuwa kinyume cha sheria, maadili mengine ya kikatiba ya utumishi wa umma kama vile usawa wa kijinsia na ushirikishaji wa watu wenye ulemavu hayakuzingatiwa,” alisema.