Habari za Kitaifa

Washirika wa Ruto na Raila waungana katika tukio adimu, kumrarua Gachagua Bungeni

Na CHARLES WASONGA October 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE wengi Jumanne walimshambulia vikali Naibu Rais Rigathi Gachagua walipojadili hoja ya kumtimua afisini wakisema mashtaka 11 dhidi yake yana mashiko.

Waliokubaliana na hoja hiyo ni washirika wa Rais William Ruto katika chama cha United Democratic Alliance (UDA) na wale wa chama cha Orange Democratic Alliance ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Waliungana na wenzao wa vyama tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza kuunga mashtaka yaliyowasilishwa na mwenzao wa Kibwezi Mashariki Mwengi Mutuse.

Huku akifafanua kila moja ya mashtaka hayo, Bw Mutuse alimsuta Bw Gachagua kwa kushusha hadhi ya afisi anayoshikilia kwa kuendeleza siasa za ukabila, migawanyiko na ubaguzi kinyume na kipengele cha 75 cha Katiba.

“Kwa kufananisha Kenya na kampuni ambayo wenye hisa nyingi ndio wanapaswa kufaidi, Naibu Rais amehujumu umoja nchini kwa kupanda mbegu za migawanyiko na ukabila,” Bw Mutuse akasema.

“Alienda katika kaunti za Kitui na Kajiado na kuwaambia kwamba hawapaswi kupewa hata wadhifa mmoja wa uwaziri. Akaenda Bungoma na kuwaambia wakazi kwamba kura walizoipa Kenya Kwanza haitoshani na nyadhifa ambazo walitunukiwa serikalini. Kisha akaenda Nandi na kuwaambia kuwa wao ndio wenye hisa wakuu katika serikali hii,” akasema.

Kulingana na Bw Mutuse kwa kuendeleza dhana hiyo potovu Bw Gachagua alidunisha afisi ya Naibu Rais ambayo ni ya kitaifa na kuchochea migawanyiko miongoni mwa makabila ya Kenya.

Mbunge huyo aliyechaguliwa kwa Chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC) pia alimhusisha Bw Gachagua na wanawe Kevin Rigathi na Keith Ikinu na uhalifu wa kiuchumi pamoja na ulanguzi wa pesa kwa kutumia washirika wao.

“Nimewasilisha ushahidi tosha wa kuonyesha kuwa Gachagua jumla ya kumpuni 22, ambazo yeye, mkewe na watoto wake wanamiliki, kuendeleza uhalifu wa kiuchumi na kufanya biashara na serikali kinyume na Katiba na sheria ya kupambana na ufisadi,” Bw Mutuse akasema.

Alitoa mfano wa mkahawa wa Treetop ulioko Nyeri akisema ni mali ya Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Nchini (KWS) lakini imekodishwa na wanawe Naibu Rais.

Kwa upande wake Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo alimsuta Bw Gachagua kwa kudai kuwa mkataba wa maelewano kuhusu ugavi wa mamlaka (MOU) kati ya vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza ndio chimbuko la dhana yake kwamba Kenya ni sawa na kampuni ya wenye hisa.

“Jumatano, nilimsikia Bw Gachagua akiendelea kudai kuwa serikali hii ni ya wenye hisa kwa misingi ya mikataba ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Ningependa kumwambia kwamba Katiba ya Kenya inayohakikisha haki na usawa kwa Wakenya wote haiwezi kudumishwa na makubaliano ya kisiasa,” akaeleza.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Owen Baya, alimshutumu Naibu Rais kwa kuichafua nchi kupitia matamshi yake ya umiliki wa hisa na kudai rasilimali zaidi kwa eneo la Mlima Kenya.

“Maelezo yake ya hisa yanatuonyesha kuwa hakuna maelewano kwenye urais, anataka kuchafua nchi hii, kama bunge tukatae,” Bw Baya alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tharaka George Murugara alisema kuwa idadi kuwa ya Wakenya waliotoa maoni yao kuhusu hoja hiyo Ijumaa na Jumamosi wiki jana walipendekeza kuwa Bw Gachagua ang’atuliwe.

“Nakubaliana na wananchi hao haswa watu wangu wa Tharaka kwamba Gachagua aondolewe. Sababu ni mashtaka yake yamethibitishwa,” akasema mbunge huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC).

Wabunge wengine waliomrarua Bw Gachagua ni pamoja na Mishi Mboko, Ruth Odinga, TJ Kajwang, Silvanus Osoro miongoni mwa wengine.