Habari za Kitaifa

Washukiwa 3 wa mauaji ya wanawake Kware kukaa ndani zaidi

Na RICHARD MUNGUTI August 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA ya Makadara imeidhinisha polisi kuendelea kuwazuia washukiwa watatu wa mauaji ya kinyama ya wanawake 17 ambao maiti yao ilipatikana katika timbo la Kware jijini Nairobi. 

Hakimu Mkazi Irene Gichobi alikubali ombi la Inspekta Patrick Wachira kuendelea kuwahoji Collins Khalusha, Amos Momanyi na Moses Ogembo hadi Agosti 26, 2024.

Bi Gichobi alifahamishwa na Inspekta Wachira kwamba polisi wamekamilisha uchunguzi wa mauaji ya watu sita ambao maiti yao imetambuliwa na watu wa familia.

“Tayari tumekamilisha uchunguzi wa waathiriwa sita ambao jamaa zao wamefaulu kutambua mili yao katika Makafani ya Nairobi,” Inspekta Wachira alimweleza hakimu.

Afisa huyo aliomba polisi wapewe siku 21 zaidi kuwawezesha kukamilisha uchunguzi wa mauaji hayo ya kutatanisha.

Maiti ya wahasiriwa hao iliguduliwa ikiwa imekatwakatwa vipande na kupakiwa ndani ya magunia na kutupwa ndani ya timbo katika eneo la Kware, Embakasi, Kaunti ya Nairobi.

Akiwasilisha ombi la kupewa muda zaidi Inspekta Wachira alisema polisi wanaendelea na kusubiri utambuzi wa mili inayohifadhiwa katika chumba cha maiti cha Nairobi.

Mchunguzi huyo wa jinai alieleza mahakama  polisi wamependekeza washukiwa hao watatu washtakiwe kwa mauaji ya wanawake hao sita.

Maiti ya wanawake hao ilipatikana katika timbo hilo.

Wananchi wakisaidiana na polisi waliopoa maiti hiyo na kupelekwa kuhifadhiwa katika makafani ya Nairobi.

Mawakili wanaotetea washukiwa hao waliomba mahakama itie kikomo uchunguzi huo kwa kuamuru mashtaka yawasilishwe dhidi ya washukiwa hao.

Mahakama ilifahamishwa kwamba haki za washukiwa hao zimeendelea kukandamizwa ikitiliwa maanani walikamatwa Julai 2024 na wangali mikononi mwa polisi.

Hakimu aliamuru washukiwa hao Collins Khalusha, Amos Momanyi na Moses Ogembo wanaodaiwa walihusika na mauaji hayo yaliyotamausha wengi, wasalie ndani hadi Agosti 26,2024 watakapoelezwa ikiwa watashtakiwa kwa mauaji au la.

Polisi waliwakamata washukiwa hao baada ya simu za baadhi ya wanawake hao waliokufa kupatikana na mmoja wa washukiwa hao.