Wasiwasi wa sukari isiyo na ladha kuzagaa madukani kwa sababu ya uhaba wa miwa
UKANDA wa Magharibi unaozalisha sukari kwa sasa unakabiliwa na uhaba wa miwa ambao umesababisha wakulima kung’ang’ania miwa ambayo haijakomaa eneo hilo.
Mamlaka inayodhibiti sukari imesema uvunaji wa miwa ambayo haijakomaa umesababisha ubora wa miwa, ambao ni kigezo muhimu katika uzalishaji wa sukari, kudorora pakubwa.
Uhaba wa malighafi hiyo muhimu inayotumika kuunda sukari umejiri miezi michache tu baada ya viwanda eneo hilo kufunguliwa tena Novemba, mwaka jana, baada ya kusimamishwa kwa miezi mitatu ili kuruhusu miwa kukomaa.
Hata hivyo, Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) katika ripoti Septemba, inaashiria siku ngumu za usoni kwa sekta ya sukari inayokumbwa na misukosuko.
“Ushindani huu umesababisha ubora wa miwa kwa jumla kudorora hasa katika eneo la Magharibi,” inasema AFA.
Data kutokana na vipimo vya miwa (CTU) vilevile inafichua kudorora kwa viwango vya chembechembe zinazoongeza utamu kwenye miwa kutoka eneo la Magharibi ambavyo vilifikia asilimia 11.37 huku Nyanza Kusini ikiongoza kwa asilimia 13.13 ikifuatiwa kwa karibu na Nyanza kwa asilimia 12.20.
Kwenye vipimo vingine muhimu kuhusu ubora, miwa kutoka Nyanza Kusini iliibuka mshindi ikiwa na viwango vya juu zaidi vya usafi bila kuingiliwa kwa asilimia 83.59 ikifuatiwa na Magharibi kwa asilimia 83.38 na Nyanza, asilimia 81.06.
AFA ilisema usafi wa miwa huenda ukachangiwa na masuala mbalimbali ikiwemo mitindo ya kuvuna, usafiri na hali ya anga ambayo inaweza kuathiri matokeo ama kwa njia hasi au chanya.
Kando na chembechembe zinazoongeza utamu kwenye miwa, AFA ilitathmini chembechembe zote zilizopo, viwango vya maji na vitu vinginevyo ili kupima ubora wa miwa kwa jumla.
“Tunapogeukia mfumo mpya wa malipo unaoegemea ubora, ni muhimu kuangazia masuala haya ili kuimarisha uzalishaji na faida katika sekta ya miwa,” ilisema ripoti.
Kama sehemu ya mpango wa serikali wa kutekeleza mfumo wa malipo ya miwa kuambatana na ubora, AFA iliweka vifaa vya kupima viwango vya ubora viwandani.
Serikali, kama sehemu ya mpango huo, imeweka vifaa hvyo katika viwanda vikuu vya sukari ikiwemo Butali, Nzoia, Mumias, na West Kenya katika eneo la Magharibi, Kibos, Chemilil, na Muhoroni vilivyopo Nyanza; na Sony Sugar, Transmara, na Sukari Industry Limited Nyanza Kusini.