‘Wataalamu’ wa ODM walioingia serikalini sasa waabudu Ruto
WANDANI wa Kiongozi wa ODM Raila Odinga, waliojiunga na serikali kama ‘wataalamu’, sasa wamegeuka watetezi wakuu wa Rais William Ruto licha ya chama chao kusisitiza walikuwa mkopo kusaidia Kenya Kwanza kukomboa nchi kutoka kwa hali ngumu kiuchumi.
Mawaziri John Mbadi (Fedha), Opiyo Wandayi (Kawi), Hassan Joho (Madini), Wycliffe Oparanya (Ushirika) na hata Kiongozi wa wachache kwenye Bunge la Kitaifa Junet Mohamed, wameanza kupuuza masaibu ya raia huku wakimpigia debe Rais Ruto achaguliwe tena mnamo 2027. Utawala wa Rais Ruto kwa sasa unakabiliwa na mawimbi makali ya kisiasa kutokwa kwa kizazi cha Gen Z na pia eneo la Mlima Kenya hasa baada ya kiongozi wa nchi kutalikiana kisiasa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua
Wandani wa Bw Odinga walipoteuliwa serikalini, waziri huyo mkuu wa zamani alisema alikubali kumpa rais ‘wataalamu’ kumsaidia kufufua uchumi wa nchi.
“Tumempa wataalamu na sasa mtaanza kuona mambo yakibadilika,” akasema Raila akihutubu kwenye soko la Toi mnamo Agosti 5.
Hata hivyo, mambo hayaonekani kuanza kubadilika kiuchumi, matatizo mengi yakiendelea kuzonga serikali na Wakenya kuanza kukata tamaa kutokana na hali ngumu huku wataalamu hao wakitetea sera za serikali walizokuwa wakipinga.
Mnamo Jumapili, Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki aliwakatisha Wakenya tamaa zaidi aliposema kuwa hali itabadilika kiuchumi baada ya miaka mitatu.
Bw Mbadi ambaye alipokezwa jukumu la kubadilisha uchumi wa nchi sasa anaonekana kugeukia siasa, akimsifu Rais Ruto na kumpigia debe kwenye eneo la Nyanza.
Waziri huyo ameonekana kulewa mamlaka kiasi kuwa ametangaza kuwa atawania urais mnamo 2032 baada ya Rais kumaliza muhula wake wa pili.
“Urais si kazi ambayo imetengewa watu wachache, hata mimi naweza na najipanga ili niwanie baada ya muhula wa Rais Ruto kukamilika,” Bw Mbadi akasema akihutubu Kaunti ya Homa Bay.
Alimiminia Rais Ruto sifa akisema akisema uongozi wake umekuwa bora zaidi kwa Wakenya wote nchini.
“Wacheni niwaambie watu wetu, kuwa serikalini si jambo baya. Juzi niliongea na Rais na akaniambia mbinu za kutumia kubuni ajira ndipo nikamweleza ni kupitia ujenzi wa viwanda vya kisasa,” akasema akiwa eneobunge la Nyando wikendi.
Bw Mbadi kabla ya kuingia serikalini alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Ruto hasa sera zake kuhusu ushuru, makato ya nyumba za gharama nafuu na bima ya afya ya kijamii.
Kwa muda wa siku mbili zilizopita, Bw Joho naye amegeuka mtetezi sugu wa Rais Ruto huku akiwajibu kwa maneno makali vijana ambao wamekuwa wakipiga Raila na Ruto vita mitandaoni
“Jana usiku (Jumatatu) walikuwa wananitumia shilingi kuniadhibu. Leo nataka kuwaambia watume pesa zaidi. Hii ndiyo nchi watu wanatumia mtandao wa kijamii kuongea vibaya kuhusu viongozi wao na kuwatabiria vibaya,” akasema Bw Joho jana Taita Taveta.
“Wanakaa kwa mtandao na hawajui mbele wala nyuma kisha wanasema Raila Odinga lazima aanguke AUC. Hawana uzalendo, wana chuki na sasa tutawakujia kwa sababu wakiharibu, tutaharibu,” akaongeza.
“Kenya haijazama, wao ndio wanazama na wakituletea noma au mbaya tutawajibu. Lazima wawe wazalendo kwa sababu hatuwezi kuwa na Kenya mbili na serikali hii ilichaguliwa kwa njia ya kidemokrasia,” akasema
Alikuwa amewarejelea Wakenya wanaotumia mtandao kukashifu utawala wa Rais Ruto kama watu wazembe na sasa wapo tayari kama serikali kuwakabili
“Kuna watu walikuwa wananiambia nikiingia serikali nitazama. Kama ni kuzama, wacha nizame nikiwa hapo ndani. Kuna watu wanafanya mpigane vita vyao na wakati walikuwa na mazuri hawakuja kwenu,” akasema akiwa Kaunti ya Tharaka Nithi Novemba 29.
Bw Wandayi naye aliapa kuwa eneo la Nyanza litaunga Rais Ruto, leo, kesho na hata milele huku akisema ni kupitia hilo tu ndipo watapata maendeleo.
Hii ni licha ya kuwa waziri huyo ‘alirukwa’ na Rais baada ya mkataba wa kukarabati uwanja wa JKIA na ule wa kuweka nyaya za umeme nchini uliopewa kampuni ya Adani kufutiliwa mbali.
Bw Wandayi alikuwa mstari wa mbele kutetea Adani na hata asubuhi kabla Rais kufuta mkataba wa Adani akihutubia Bunge, waziri huyo alitetea kampuni hiyo iliyozongwa na ufisadi kwenye mataifa ambayo imewahi kutelekeleza miradi
“Kama jamii, tumeamua kufanya kazi na Rais Ruto tukiwa ndani, leo, kesho na hata siku za baadaye. Ni matumaini yetu kuwa hakutatokea uchaguzi mwingine ambao serikali itabuniwa bila watu wetu,” akasema Bw Wandayi.
“Hii serikali jumuishi imewaleta watu pamoja na ikifika 2027 tutakuja pamoja jinsi tulivyo. Kwa sasa tutasaidiana kujenga nchi hii na Rais Ruto na nashukuru Raila kwa kuniingiza ndani ya serikali ili tufanye kazi na Rais,” akasema Waziri wa Vyama vya Ushirika na Mikopo Wycliffe Oparanya
Mdadisi wa masuala ya kisiasa Profesa Macharia Munene anasema viongozi wa ODM wamekerwa na jinsi umaarufu wa Bw Gachagua na lazima waonyeshe juhudi za kujitambulisha
“Wanakula kwa Ruto na pia hawataki kuachilia upinzani na sifa ambayo walikuwa nayo kama ya kutetea raia sasa imechukuliwa na Gen Z ambao wameshinda wakiwakosoa mitandaoni,” akasema Profesa Munene.
“Njia moja ya kumaliza ushawishi wa vijana ni kurejelea siasa ya zamani ambazo ODM inataka. Kwa sasa pia hawataki kukosana na Rais Ruto kwa sababu hawataki eneo la Mlima Kenya lirejee serikalini kwa hivyo lazima wamfurahishe ndiyo maana kazi yao ni kusema ‘ndio’,” akaongeza mhadhiri huyo.
Junet naye amekuwa akiandamana na Rais Ruto maeneo mbalimbali na Jumanne Taita Taveta alisema mikutano ya ushirikishaji wa umma inastahili kuondolewa ili Rais afanye kazi jinsi anavyotaka.
“Hili hitaji la kuomba ruhusa kuhusu kila kitu lazima iondolewe. Serikali inachaguliwa na raia ilhali inahitajika kuomba ruhusu kutoka kwa Wakenya, viongozi wa mashirika, bunge, mahakama. Hali ikiwa hivi serikali itafanya kazi lini?” akauliza Bw Mohamed, kauli iliyowakasirisha Wakenya.