Habari za KitaifaMakala

Watatu waliotekwa nyara Kitengela wamepatikana Kiambu

Na CHARLES WASONGA, LABAAN SHABAAN September 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WATU watatu waliotekwa nyara Kitengela mwezi mmoja uliopita wamepatikana wakiwa hai, Rais wa Chama cha Mawakili (LSK) Faith Odhiambo amesema.

Ndugu wawili Jamil Longton (42) na Aslam Longton (36) walipatikana Gachie Ijumaa asubuhi.

“Ninaarifiwa kuwa Jamil Longton na kaka yake Aslam walitupwa Gachie katika mpaka wa Kiambu na Nairobi. Kila ombi na juhudi zilisaidia. Tunashukuru Mungu kuwa wako salama,” Bi Odhiambo alisema kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X.

Walikuwa wametekwa nyara pamoja na mshirikishi wa vuguvugu la FreeKenya Movement Bob Njagi ambaye pia amepatikana akiwa hai eneo la Tigoni, Kaunti ya Kiambu.

Babake Longman Njagi amethibitisha; “Nilipigiwa simu jana usiku (Alhamisi) na kuambiwa na polisi wa kituo cha  Tigoni kuwa mwana wangu amepatikana akiwa hai.”

Polisi walisema nini?

Inspekta Jenerali mpya wa Polisi Douglas Kanja alisema watu watatu waliodaiwa kutekwa nyara  mjini Kitengela Agosti 19, 2024 hawazuiliwi na polisi.

Akiongea na wanahabari , Alhamisi, Septemba 19, 2024 muda mfupi baada ya kuapishwa rasmi, Bw Kanja aliomba umma usaidie polisi katika juhudi za kuwasaka watatu hao.

“Mwafahamu kwamba wakati huu ndio nimeingia afisini. Lakini ningependa kusema kuwa habari ambazo nimepata kutoka kwa maafisa wetu ni kwamba hatujawazuilia watu hao watatu kutoka Kitengela. Ninachojua ni kwamba ripoti kuhusu kutoweka kwao iliwasilishwa na uchunguzi unaendelea,” Bw Kanja akawaambia wanahabari nje ya jumba la Jogoo, Nairobi.

Inspekta huyo Jenerali alikuwa ameandamana na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin pamoja na maafisa wengine wakuu wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).

Watatu hao ni; Longton Jamil (42), kakake Aslam Longton (36), na mshirikishi wa vuguvugu la FreeKenya Movement Bob Njagi, walitoweka mnamo Jumatatu  Agosti 19, 2024 baada ya kutekwa nyara kwa nguvu na watu waliodaiwa kuwa maafisa wa polisi.

Ripoti zinasema kuwa kaka hao wawili walitekwa nyara mita chache kutoka nyumbani kwao.

Naye Bw Njagi alidaiwa kutolewa kwa nguvu kutoka ndani ya basi moja eneo la Mlolongo na watu wasiojulikana waliomwingiza ndani ya gari moja aina ya Subaru na wakatoweka naye.

Vuguvugu la FreeKenya Movement linaamini kuwa kutekwa nyara kwa Njagi kunahusiana na hatua yake ya kumtetea mfanyabiashara Jimi Wanjigi alipokamatwa na polisi na kisha akazuiwa katika kituo cha Kamukunji, Nairobi.

Kufuatia kutoweka kwa watatu  hao Chama cha Mawakili Nchini (LSK) na shirika la Katiba Institute ziliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi zikitaka polisi waseme waliko na wawasilishwe kortini ili wafunguliwe mashtaka kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara saba Jaji wa Mahakama hiyo Lawrence Mugambi alimtaka aliyekuwa Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli afike kortini kuelezea waliko watatu hao lakini akakaidi.

Mnamo Ijumaa wiki jana Jaji Mugambi alimhukumu Masengeli kifungo cha miezi sita gerezani kwa kosa la kukaidi agizo la mahakama.

Sasa Masengeli anatarajiwa kufika kortini Ijumaa, Septemba 20, 2024 kujitetea dhidi ya hukumu hiyo.