Habari za Kitaifa

Watatu watafutwa boti ikizama kwenye mashindano baharini, 22 wanusurika

Na  WACHIRA MWANGI October 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Hofu imetanda kufuatia tukio la kusikitisha ambapo watu watatu wanahofiwa kufariki baada ya boti ya mashindano iliyokuwa na washiriki 22, kuzama wakati wa tamasha la East Africa Ocean Festival (TEAOF) 2025 katika Tudor Water Sports Club, Mombasa, Ijumaa jioni.

Watu 19 waliokolewa kwenye mkasa huo uliotokea karibu kabisa na mstari wa mwisho wa mbio hizo za boti. Ripoti za awali zinaonyesha kuwa boti hiyo ilikuwa mojawapo ya tatu zilizokuwa zikishiriki katika mashindano hayo.

Afisa Mkuu wa Zimamoto katika Kaunti ya Mombasa, Bw Ibrahim Basafar, alisema tukio hilo lilitokea mwendo wa saa kumi na moja na nusu jioni boti hiyo ilipozama.

“Operesheni ya uokoaji ilianza mara moja na tuliweza kuwaokoa watu 19, wawili kati yao wanahitaji msaada wa kisaikolojia kutokana na mshtuko. Mshiriki mmoja aliyekuwa katika hali mahututi alikimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Pwani,” alisema Bw Basafar.

Bw Basafar alithibitisha kuwa watu watatu bado hawakuwa wamepatikana kufikia Ijumaa usiku.

“Kutoka kwenye eneo letu la kusaidia manusura, tunathibitisha kwamba bado watu watatu hawajulikani walipo,” aliongeza.

Jumamosi asubuhi, waokoaji walisema walipata mili miwili baharini na walikuwa katika harakati za kuiopoa,

Kikosi cha dharura kinachojumuisha Serikali ya Kaunti ya Mombasa, Huduma ya Walinzi wa Pwani wa Kenya (KCGS) na mashirika mengine ya usalama, kinashiriki operesheni hiyo.

Bw Basafar aliwataka wananchi kuwa watulivu na kutoingilia kazi ya wahudumu wa dharura.

“Sisi ni waokoaji wa maisha na mali, lakini bado tunashambuliwa. Nani atakusaidia ukiwa hatarini? Wahudumu hawa wako hapa kusaidia,” alisema, baada ya gari la wagonjwa mahtuti kuripotiwa kuvunjwa na baadhi ya jamaa na mashabiki waliokuwa na hasira.

Walioshuhudia  walieleza kuwa hali ilikuwa ya mtafaruku mkubwa, huku jamaa wa waathiriwa na washiriki waliokuwa wamesongwa na huzuni na hofu, wakirusha mawe na kuharibu mali katika eneo hilo.

Kulingana na mmoja wa washiriki walionusurika, mkasa huo ungeepukwa iwapo tahadhari za usalama zingekuwa zimezingatiwa.

“Hakuna hata mmoja wetu aliyekuwa na jaketi ya usalama wakati wa mashindano,” alisema Bw Ishmael Onyango, manusura na mshiriki wa timu ya Kijiweni Uplifters kutoka mtaa wa Bangladesh, Mombasa.

“Tulialikwa kushiriki kwenye mashindano haya na tumekuwa tukifanya mazoezi tangu Jumatatu. Tulikuwa tukitumia maboya wakati wa mazoezi, lakini siku ya mashindano, ni timu moja tu iliyokuwa nayo. Tulikuwa karibu sana na mstari wa mwisho ndipo boti yetu ikazama. Kila kitu kilitokea kwa haraka mno,” alisimulia.

Bw Onyango aliongeza kuwa waandalizi wa hafla hiyo hawakuwa wamewasiliana nao tangu mkasa utokee.

“Tulikuwa 22 ndani ya boti, na wale watatu waliopotea ni wachezaji wetu. Familia zao sasa zimeanza kutupigia simu, tutawaambia nini?” alihoji kwa masikitiko.

Waziri wa Ardhi na Mipango ya Miji wa Kaunti ya Mombasa, Bw.Hussein Mohammed, ambaye pia alikuwepo eneo la tukio, alisema juhudi zinaendelea kuwatafuta waliopotea.

“Tunashirikiana na maafisa wa KCGS, wakiwemo wapiga mbizi. Pia tunakagua sajili ya washiriki ili kubaini majina ya waliopotea,” alieleza.

.