Wazazi walia walimu wakitimua wanafunzi kwa kukosa karo
MATUMAINI ya wanafunzi kurejelea masomo yao baada ya kumalizika kwa mgomo wa walimu wa wiki moja yamekatizwa kufuatia matakwa ya baadhi ya wakuu wa shule kutaka karo yote ilipwe kabla ya wanafunzi kuingia darasani.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Dijitali ulibaini kuwa wakuu wengi wa shule wametoa maagizo kwamba hakuna mwanafunzi anayepaswa kuruhusiwa shuleni bila kulipa karo yote ikiwa ni pamoja na ada za kuwapa motisha walimu.
Baadhi ya shule zilizowarudisha wanafunzi nyumbani Jumanne, Septemba 3, 2024 ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loise Nanyuki, Shule ya Upili ya Tigithi na St Jude’s Ntrukuma.
Wanafunzi katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Nanyuki walitazamiwa kurejea kusoma siku ya Alhamisi, Septemba 5, 2024 lakini wazazi ambao hawajalipa pesa zote walikuwa wameonywa wasiwarudishe shuleni.
“Nina salio la karo la Sh23, 000 lakini nimefanikiwa kupata Sh5, 000 pekee kwani nilikuwa nimelipa Sh10, 000 wiki jana mwanzoni mwa muhula wa tatu. Mwanangu ambaye anafanya mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) ameripoti hata nikiwa na salio hilo kubwa la karo kwa vile ninahisi kuwa si haki kuwaadhibu wanafunzi wa kidato cha nne katika wakati huu muhimu,” akasema mzazi kutoka Othaya, Kaunti ya Nyeri ambaye alikataa kutajwa jina akihofia kuwa mtoto wake anaweza kudhulumiwa.
Mzazi huyo ambaye ni mama asiye na mume, alisema Shule ya Upili ya Wavulana ya Nanyuki inatoza Sh3, 500 kila muhula kwa mwanafunzi kama ada ya motisha ambayo wasimamizi wa shule wanashikilia kwamba pesa hizo zilipwe zote kabla ya wanafunzi kuruhusiwa kuingia shuleni.
Wakuu wa shule wanasema kuwa ada hizi, hutumika kulipa walimu wanaojitolea muda wao kufundisha nje ya saa rasmi za kazi.
Walimu walioajiriwa na Bodi ya Usimamizi wanasemekana kupata malipo yao ya kila mwezi kutoka kwa pesa hizi.
Mzazi mwingine kutoka Shule ya Sekondari ya Loise Nanyuki alisema amelipa karo yote lakini shule bado inadai Sh9, 000 za mradi wa basi kabla ya binti yake kurudi shuleni.
“Binti yangu aliripoti Jumatano (Septemba 4, 2024) na hakuruhusiwa shuleni kwa vile sijalipa pesa za mradi wa basi. Wakuu wa shule wanafaa kuwa waangalifu ili wasiadhibu watahiniwa wa KCSE kwa sababu ya miradi isiyohitaji kipaumbele wakati wana takriban mwezi mmoja kabla ya kufanya mtihani wa kitaifa na ikikumbukwa tayari wamepoteza wiki mbili kufuatia mgomo wa walimu,” akasema mzazi huyo.
Maoni kama hayo yalitolewa na wazazi wa Shule ya Wavulana ya Tigithi ambao watoto wao waliripoti Jumatano lakini wakarudishwa siku iliyofuata kuchukua karo.
Mgomo wa walimu ulioitishwa na Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vyuo vya Kadri (Kuppet) ulitatiza masomo kwa wiki moja kabla ya maafisa wa chama hicho kuwataka wanachama kurejea kazini Jumatatu iliyopita.