Wetang’ula ahimiza vijana kujisajili kupiga kura, asifu uajiri wa walimu
WITO umetolewa kwa Wakenya, hususan vijana, kujitokeza kwa wingi na kujisajili kuwa wapiga kura ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, alitoa wito huo alipohutubia waumini katika ibada ya Family Day iliyofanyika Kanisa Katoliki la Mutuati, Kaunti ya Meru.
“Tuna zaidi ya miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu. Vijana, sasa ndio wakati wa kujitayarisha mapema kwa kupata vitambulisho vya taifa na kujisajili kama wapiga kura,” alisema.
Wetang’ula alisema ushiriki wa vijana katika uchaguzi ni muhimu kwa mustakabali wa taifa na kwa kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa wanawakilisha kwa haki sauti ya kizazi kipya.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikitarajiwa kuanza kampeni ya kitaifa ya usajili wa wapiga kura baada ya makamishna wapya kuteuliwa na kuanza kuchapa kazi.
Bw Wetangula alisifu kwa dhati hatua ya serikali ya Rais William Ruto kuwekeza pakubwa katika sekta ya elimu kupitia kuajiri walimu,
“Tangu Rais Ruto aingie madarakani, zaidi ya walimu 76,000 wameajiriwa. Bajeti ya sasa imetenga fedha kwa ajili ya kuajiri walimu wengine 24,000, na hivyo kufikisha jumla ya walimu 100,000 katika kipindi cha miaka mitatu tu. Hili halijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi yetu,” alisema.
Spika huyo alieleza kuwa hatua hiyo imesaidia kupunguza idadi ya wanafunzi kwa kila mwalimu darasani, kuboresha ubora wa elimu, na kuwahakikishia wanafunzi waliobobea na wenye motisha ya kuwafundisha.
Katika hotuba yake, Spika huyo alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa upinzani ya kukosa heshima kwa viongozi wa serikali, na akahimiza utamaduni wa kisiasa wa kuheshimiana na kuwa na nidhamu.
“Ili uongozi uwe na maana, lazima uanzie na tabia njema na heshima. Huwezi kutaka kuheshimiwa ikiwa wewe huwaheshimu wengine,” alisema.
Pia alikosoa maandamano ya vurugu akisema yanarudisha nyuma maendeleo na kuongeza tatizo la ukosefu wa ajira. Alisisitiza kwamba elimu na ujuzi kwa vijana ni njia bora ya kushughulikia.