Wezi wa mifugo wameanza kuvaa sare za polisi
MAJANGILI wanaoogopwa sasa wanavaa sare za polisi kutekeleza mashambulizi mapya na wizi ukiwemo wa mifugo, huku maafisa wa usalama sasa wakiwasaka wanaowauzia sare hizo baada ya wananchi kuwapashwa kuwahusu.
Vikundi vya usalama vya mashirika tofauti pia vinatafuta usaidizi kutoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CAK) ili kuimarisha mtandao katika maeneo hatari kwa ujangili kusaidia katika kuwasaka majangili hao.
Kamati ya Usalama ya Kaunti ya Turkana kwa sasa inachunguza wafanyabiashara ambao wanawauzia majangili na wahalifu sare za polisi zilizotumika kuwezesha shughuli zao haramu.
Kulingana na Kamishna wa Kaunti Julius Kavita, wakati mwingine majangili huwa wanatumia mili ya maafisa wa polisi wanaouawa wakati wa mashambulizi kuiba silaha na sare zao.
Alisema tayari timu ya usalama ya kaunti imeweza kutwaa sare 16 za Huduma ya Kitaifa ya Polisi.
Operesheni Maliza Uhalifu iliyozinduliwa Februari 2023 na Wizara ya Usalama wa Ndani imeboresha kwa kiasi kikubwa hali ya usalama katika vijiji vya mpakani katika Kaunti Ndogo za Turkana Mashariki na Turkana Kusini ambazo zilitangazwa kwenye gazeti la serikali kama hatari.
Hili linathibitishwa na kutotatizika kwa usafiri kwenye barabara ya Kapenguria – Lodwar, hasa katika sehemu kati ya Kalemngorok na Marich Pass ambayo yaliwahi kukumbwa na mashambulio ya mara kwa mara ya majangili.
Haya yamefanikishwa na amri ya kutotoka nje jioni hadi alfajiri na doria za maafisa wa usalama kutoka Huduma ya Polisi na Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, (KDF).
Ingawa maafisa wa usalama wana vifaa na silaha za hali ya juu kwa ujasusi wa eneo hilo linalokumbwa na ukosefu wa usalama, wahalifu hao bado wanafaidika kwa kufahamu hali ya kijiografia yenye miamba na ya milimani.
Habari mpya zaidi ni kwamba majangili walio na silaha haramu na wanaodhaniwa kuwa na silaha za kisasa wanavalia sare za maafisa wa polisi.
‘Tunachunguza visa ambapo wahalifu wenye silaha wanavalia sare za polisi katika vijiji vilivyo katika maeneo yenye utovu wa usalama. Katika vijiji kama hivyo, wenyeji wasiojua kusoma na kuandika hata wanadanganywa kukabidhi mifugo kwa hiari wakiaambiwa ni kwa usalama wao,” alisema Kamishna wa Kaunti ya Turkana Kavita.
Alisema kupitia taarifa kutoka kwa wananchi walifanikiwa kunasa sare 16 za Polisi katika magari ya uchukuzi wa umma ambazo zilikuwa zikipelekwa kituo cha Kalemng’orok ambacho pia kimekumbwa na matukio ya ujangili.
Bw Kavita alionya maafisa wa polisi dhidi ya kuwauzia wahalifu sare ili kusaidia katika juhudi za kukabiliana na ukosefu wa usalama.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Turkana Daniel Kinyua alisema kuwa kamati ya usalama ya kaunti hiyo inatafuta usaidizi kutoka kwa CAK ili kuimarisha mtandao katika maeneo ambayo hayana na ambayo hukumbwa na ujangili ili wenyeji waweze kutoa habari za kijasusi kwa urahisi.